Kocha mpya kijana kumsaidia Capello

Image caption Capello amesema ataelekeza nguvu zaidi kuendeleza wachezaji vijana.

Meneja wa timu ya England, Fabio Capello, amekubali kuteua kocha kijana ambaye ni mzawa wa England ajumuike na Stuart Pearce kwenye kikosi chake cha ufundi, BBC Sport imefahamishwa.

Mkurugenzi wa maendeleo wa chama cha soka cha England, Sir Trevor Brooking, amesema atasaidia kuteua kocha huyo na kuwasilisha mapendekezo yake ifikapo mwezi Disemba.

Pearce, ambaye pia ndiye kocha wa timu ya England ya wachezaji wa chini ya umri wa miaka 21, tayari yumo katika kikosi cha makocha cha Capello.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya bodi ya FA kukutana kujadili ufanisi mbovu wa timu ya England kwenye mashindano ya Kombe la Dunia.

Nafasi kwa vijana

Mwandishi wa maswala ya michezo wa BBC, Dan Roan alisema: "FA inataka Brooking na Capello kutafuta kocha mwingine kijana kusaidia katika kikosi cha ufundi cha timu ya taifa ya England, bega kwa bega na Stuart Pearce.

Wawili hao watawasilisha mapendekezo yao kuhusiana na mpango wa kuendeleza wachezaji wa kimataifa na mafunzo ya makocha, huku chama cha soka, FA, kikiwa na shauriku ya kujifunza kutokana na England iliyokuwa ikimwagiwa sifa, kushinda mechi moja tu.

Capello, ambaye aliendelea na kazi yake baada ya mashindano, alisema ataelekeza zaidi nguvu zake kuendeleza wachezaji vijana. Hatua za kwanza zitaanza kuonekana wakati England itakapocheza na Hungaru katika mechi ya kirafiki kwenye uwanja wa Wembley, tarehe 11 Agosti.