Fifa yaibana Sudan

Shirikisho la soka la kimataifa Fifa, limeipa Sudan hadi Agosti 15 kurudia kufanya uchaguzi wa chama cha soka cha nchi hiyo, la sivyo kitafungiwa kushiriki michuano yoyote.

Image caption Kamal Shaddad

Fifa imesema haitambui uchaguzi uliofanyika hivi karibuni wa chama cha soka cha Sudan SFA ambao ulifanyika Julai 26.

Mutasim Jaafar alichaguliwa kuwa rais mpya wa chama, kwenye uchaguzi huo.

Fifa haijafurahishwa na hatua ya serikali ya Sudan kumpiga marufuku kiongozi wa zamani wa SFA Kamal Shadda kuwania muhula wa tatu.

Sudan kufungiwa

"Kamati ya masuala ya dharura ya Fifa imeamua kutotambua matokeo ya uchaguzi huo, na kutoa tarehe ya mwisho ya Agosti 15, kufanya upya uchaguzi kwa mujibu wa kanuni za SFA na bila kuingiliwa na yeyote" imesema taarifa kutoka Fifa.

Uwezekano wa Sudan kufungiwa unaweza kusababisha kushindwa kucheza mchezo wa ufunguzi wa michuano ya kufuzu kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Congo Septemba 3.

Mismamo wa Fifa

Katibu mkuu wa SFA Majdi Shamseddin amesema chama hicho kitafanya mkutano wa dharura siku ya Jumanne ili kujadili msimamo wa Fifa.

"Tutajitahidi kufanya kila tuwezalo kukabiliana na hali hii, na pia kuepuka mkanganyiko wowote na Fifa, SFA na serikali ya Sudan," Majdi ameliambia shirika la habari la Reuters.

Shamseddin amesema sheria inayomzuia rais wa zamani kugombea, ni sheria ya Sudan na haijajumuishwa kwenye kanuni za SFA, na ndio maana Fifa imepinga.

Uamuzi wa mwisho

Amesema njia moja ya kutatua suala hilo ni kwa Mkutano Mkuu wa SFA kupiga kura kuamua kuingiza kipengele hicho ndani ya katiba ya SFA, lakini hata hivyo amesema uamuzi wa mwisho utafikiwa katika mkutano wa Jumanne.

Baraza la michezo la taifa limekataa kusema lolote kuhusu suala hilo.