Fabregas mbioni kubakia Emirates

Image caption Cesc Fabregas alianzia soka yake Barcelona, lakini sasa ni vita dhidi ya Arsenal wanaotaka abakie na timu hiyo ya London.

Klabu ya Arsenal inaonekana kushinda katika vita vyake vya kummiliki kumhodhi nahodha wake Cesc Fabregas.

Kwa kipindi cha likizo ya ligi kuu ya England na kupitia kipindi cha Kombe la Dunia, mchezaji huyo amekuwa chachu ya mvutano kati ya Arsenal na kule alikoanzia kucheza mpira Barcelona.

Barcelona iliwasilisha ombi la kumtaka mchezaji huyo ahamie kwao kwa kutoa kitita cha pauni milioni 30 kilichokataliwa mnamo mwezi Juni.

Rais wa klabu ya Barcelona, Sandro Rosell, pamoja na wachezaji wake wametumia njia mbalimbali kumshawishi meneja wa Arsenal abadili mawazo yake kwa kumuacha kiungo huyo ahamie kwao.

Mapema wiki hii, kijana huyo alionekana kuzidisha moto alipouambia umati wa watu 2,500 wa kijijini kwao kuwa ana matumaini ya kuwaona mara kwa mara ikiashiria kuwa labda kwa sababu atakuwa akichezea timu ya Barcelona ndani ya Hispania.

Licha ya yote hayo, moyo na imani ya Arsene Wenger pamoja na mashabiki wa Arsenal utakuwa umetulia baada ya kijana huyo mwenye umri wa miaka 23 kurudi kwenye uwanja wa Emirates kwa mazoezi na wachezaji wenzake wa msimu uliopita.

Kwenye uwanja wa Emirates kushuhudia mazoezi na picha ya kwanza msimu huu, walikuwepo mashabiki 7,000 miongoni mwao akiwemo nahodha wa zamani wa klabu hiyo Kenny Samson aliyewaambia wandishi wa habari kuwa: "Nimezungumza na Arsene Wenger na amenihakikishia kuwa Fabregas ataichezea Arsenal."