Fabregas atuliza nyoyo Emirates

Klabu ya Arsenal inaonekana kushinda katika vita vyake vya kumhodhi nahodha wake Cesc Fabregas.

Image caption Francesc Fabregas

Mchezaji huyo amekuwa chachu ya mvutano kati ya klabu yake ya Arsenal na ile alikoanzia kucheza mpira, Barcelona kwa kipindi cha mapumziko ya Ligi kuu na kipindi cha Kombe la Dunia.

Barcelona iliwasilisha ombi la kumtaka mchezaji huyo ahamie kwao kwa kutoa kitita cha pauni milioni 30 kilichokataliwa mnamo mwezi juni.

Image caption Cesc Fabregas arejea mazoezini Emirates

Rais wa klabu ya Barcelona Sandro Rosell pamoja na wachezaji wa klabu hiyo wametumia njia mbalimbali kumshawishi Meneja wa Arsenal abadili mawazo yake na kumruhusu kiungo huyo ahamie Barca.

Mapema wiki hii kijana huyo alionekana kuzidisha moto alipouambia umati wa watu 2500 wa kijijini kwao kuwa anatumaini kuwaona mara kwa mara hali iliyoashiria kuwa huenda akarejea kusakata soka nchini Uhispania.

Image caption Pepe Reina akiwa na Fabregas

Licha ya yote hayo, nyoyo na imani ya Arsene Wenger pamoja na mashabiki wa Arsenal zitakuwa zimetulia baada ya kijana huyo mwenye umri wa miaka 23 kurudi kwenye uwanja wa Emirates kwa mazoezi na wachezaji wenzake wa msimu uliopita.

Image caption Fabregas

Kwenye uwanja wa Emirates kushuhudia mazoezi na kupiga picha za kwanza za msimu huu, walikuwepo mashabiki 7,000 miongoni mwao akiwemo nahodha wa zamani wa klabu hiyo Kenny Samson aliyewambia wandishi wa habari kuwa, 'nimezungumza na Arsene Wenger na amenihakikishia kuwa Fabregas ataichezea Arsenal.'