Man U yabanwa, Newcastle yaangamiza

Brede Hangeland alilipa deni kwa timu yake baada ya kupiga mpira kwa kichwa uliozaa goli la kusawazisha, wakati Fulham ikicheza na Manchester United, kabla ya hapo Hangeland alikuwa amejifunga mwenyewe kuizawadia Man U goli la pili.

Image caption Wachezaji wa Fulham wakimpongeza Brede Hangeland baada ya kuipatia timu yake goli la kusawazisha na kuokoa pointi moja.

Matokeo hayo yamevuruga mipango ya Manchester United kupata ushindi wa pili mfululizo tangu kuanza kwa michuano ya ligi kuu msimu huu.

Awali, kunako dakika ya 10 kipindi cha kwanza, Paul Scholes alitandika mkwaju wa mita 25 kuipatia United goli la kuongoza, ingawa Simon Davies alisawazisha kutoka miguu 12.

Katika shambulio kali la United, Hangeland alijifunga mwenyewe wakati kona ilipomzidia na United wakawa mbele kwa magoli mawili.

Hata hivyo United watajilaumu wenyewe kwa kushindwa kutumia penati ambayo ilipigwa na Nani kisha kupanguliwa na mlinda mlango David Stockdale dakika chache baadaye.

Hangeland aliruka juu kwa nguvu kudonyoa mpira wa kona na kuiwezesha United kuondoka na pointi moja.

Newcastle United dhidi ya Aston Villa

Katika mechi ya kwanza kati ya mbili siku ya Jumapili, Newcastle United waliorejea upya Ligi Kuu ya Soka ya England, walitoa kipigo cha mwizi kwa kuitandika Aston Villa magoli 6-0.

Villa ambao waliondokewa na kocha Martin O'Neil siku chache kabla ya msimu kuanza, walizidiwa kwa kila hali na kuwapa nafasi Newcastle kung'ara kwa kiasi kikubwa na kuondoa machungu ya kupoteza mechi ya kwanza dhidi ya Man United juma lililopita.

Katika mpambano huo, Andy Carroll alifunga magoli matatu wakati Kevin Nolan alifunga mawili.

Ukali wa washambuliaji wa Villa ulisababisha penati katika dakika ya tisa, lakini John Carew alipaisha mkwaju wake na baada ya hapo ikawa zamu ya Newcastle kuiangamiza Villa.

Wafungaji.

  • Barton 12
  • Nolan 31
  • Carroll 34
  • Carroll 67
  • Nolan 87
  • Carroll 90+3

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii