Rudisha avunja rekodi tena

David Rudisha
Image caption Amevunja rekodi mara mbili katika kipindi cha wiki moja

Mkenya David Rudisha kwa mara ya pili katika juma moja, ameivunja rekodi ya dunia ya mbio za mita 800.

Wakati huu ameandikisha muda wa dakika moja, sekunde 41,01 katika mashindano ya Rieti, nchini Italia, Jumapili, tarehe 29 Agosti 2010.

Jumapili iliyopita, Rudisha, mwenye umri wa miaka 21, alikuwa ameandikisha rekodi mpya ya dakika moja, sekunde 41.09, na kufutilia mbali rekodi ya Wilson Kipketer, ambayo ilikuwa imedumu kwa muda wa miaka 13.

Mwaka jana, katika mashindano hayo ya Rieti, Rudisha alikuwa ameandikisha rekodi mpya ya bara la Afrika katika mbio hizo.

Ingawa alifika tu nusu-fainali za mashindano ya dunia mwaka 2009, Rudisha amekuwa akiimarisha muda wake, na hatimaye kufanikiwa kuiondoa rekodi ya Kipketer.

Mara tu baada ya kufanikiwa kufanya hivyo, alisema hiyo ilikuwa ndio juhudi ya kwanza katika kujaribu kuivunja rekodi ya ulimwengu, na aliahidi kuongeza kasi.

Mkenya mwenzake, Boaz Kiplagat Lalang alishikilia nafasi ya pili.

Mmarekani Nick Symmonds, alikuwa wa tatu katika muda wa dakika moja, sekunde 43.76.