Wenger akiri utovu wa nidhamu

Arsene Wenger
Image caption Ni kawaida siku hizi kwa Wenger kuonyesha hasira mambo yanapokwenda kombo

Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, ametozwa faini ya dola 12,500 au pauni 8,000 kwa kukosa nidhamu alipomwandama mmoja wa wasimamizi wa mechi kati ya Arsenal na Sunderland ambapo Sunderland walisawazisha mnamo sekundi za mwisho wa muda wa ziada. Shirika la Kandanda la Uingereza, FA, pia limemfungia Wenger mechi moja, hatua ambayo itamfanya akose pambano la Jumanne la kombe la Carling dhidi ya Tottenham Spurs. Kwa mujibu wa taarifa ya FA, Wenger alikubali kulipa faini hiyo baada ya kukiri makosa yake.

Meneja huyo alikerwa wakati mshambulizi wa Sunderland, Darren Bent alifunga bao la kusawazisha mnamo dakika ya 95 huku mechi hiyo ikiwa imekadiriwa kuisha mnamo dakika ya 94.

Fabregas

Na wakati Wenger akijikuna mfukoni huenda akapata kituliza roho kufuatia taarifa kwamba nahodha wa timu yake Cesc Fabregas hakujeruhiwa vibaya kama ilivyohofiwa.

Fabregas ametoa taarifa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter akisema ana matumaini ya kurejea uwanjani mnamo wiki mbili zijazo.