Liverpool yalemewa na Everton 2-0

Wamiliki wapya wa Liverpool
Image caption Huenda wakati wa Hodgson kucheka umekwisha

Kiza kimetanda Liverpool baada ya kutandikwa mabao 2-0 na mahasimu wao wa jadi Everton kwenye uwanja wa Goodison park.

Bao la kwanza la Everton lilipachikwa na Tim Cahill mnamo dakika ya 34 ya kipindi cha kwanza.

Baada ya mapumziko, hata kabla ya Liverpool kujipanga vizuri, Mikel Arteta alisukuma wavuni bao la pili mnamo dakika ya nne. Matokeo hayo yalikuwa pigo kubwa kwa wamiliki wapya wa Liverpool.

Mnamo kipindi cha pili Liverpool walijaribu mbinu mbali mbali lakini hawakuona lango la Everton.

Bila shaka kutakuwa na maswali magumu katika ngome ya Liverpool sio tu kuhusu matokeo hayo bali pia kuhusu baadhi ya wachezaji wake.

Kwa mfano mshambulizi Fernando Torres hakuonyesha mikiki na machachari ambayo huwatisha wapinzani.

Katika mechi hii, alionekana mnyonge ila mara moja tu aliposukuma mkwaju lakini ukaokolewa.