Alonso aongoza katika kuwania ubingwa

Fernando Alonso
Image caption Alonso anaongoza hivi sasa katika kuwania ubingwa msimu huu

Dereva wa timu ya Ferrari, Fernando Alonso, anaendelea kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa dunia, baada ya kupata ushindi katika mashindano kwanza ya magari ya Grand Prix kufanyika Korea ya Kusini.

Muingereza Lewis Hamilton, dereva wa McLaren, alishikilia nafasi ya pili, na dereva mwingine wa Ferrari, Felipe Massa kutoka Brazil, alimaliza katika nafasi ya tatu.

Bingwa mtetezi Jenson Button kutoka Uingereza, wa timu ya McLaren, alimaliza katika nafasi ya 12, na akipoteza matumaini yote ya kupata ubingwa msimu huu.

Alonso sasa anaongoza katika kuwania ubingwa msimu huu, akimtangulia mpinzani wake mkali sana, Mark Webber wa timu ya Red Bull, kwa pointi 11.

Webber alilazimika kujiondoa mapema kutoka mashindano hayo baada ya gari lake kupata ajali.

Alonso amemuacha nyuma dereva wa Uingereza, Hamilton, kwa pointi 21.

Vettel, ambaye alifuzu kuanza mashindano ya Jumapili katika nafasi ya kwanza, sasa ameachwa nyuma na Alonso kwa pointi 25, baada ya gari lake kuwa na matatizo ya injini.

Huku ikiwa ni mashindano mawili tu yaliyosalia kuamua mshindi msimu huu, Alonso amesema hamna mabadiliko makubwa katika kuwania ubingwa.

"Tunafahamu katika utaratibu mpya wa kupata pointi mabadiliko mengi yanaweza kujitokeza katika shindano moja - ikiwa hutapata pointi, basi utapoteza pointi zote 25 kwa wapinzani wako", alielezea dereva huyo kutoka Uhispania.