SAMUEL ETO'O

Etoo
Image caption Samuel Eto'o

Mwaka huu, nyota ya Samuel Eto'o ilizidi kung'ara alipocheza katika timu iliyoshinda taji la klabu bingwa barani ulaya kwa mara ya tatu. Eto'o alikuwa akichezea Barcelona mwaka wa 2006 na 2009 waliposhinda taji hili, na ushindi wa Inter Milan unamaanisha mchezaji huyu kutoka Cameroon ameweza kushinda taji hilo mfululizo akichezea timu tofauti.

Bofya hapa kupiga kura:

Bila shaka mchezaji huyu ameshinda taji nyingi , ikiwa ni pamoja na zile tatu akiwa club ya Inter Milan iliposhinda kombe la klabu bingwa barani ulaya na ligi ya Italia.

Ushindi huu umetokea katika mwaka mmoja tu baada ya ushindi mwingine sawa na huo akichezea timu ya Barcelona. Eto'o ni mchezaji wa kwanza kupata ushindi wa aina hii.

Mchezaji huyu alionyesha umahiri wake alipocheza katika nafasi isiyo yake ya kawaida na akaweza kufunga bao lililowabandua Chelsea kutoka mashindano hayo ya bara ulaya mwezi Machi.

Image caption samuel Eto'o

Baada ya Rafael Benitez kuchukua nafasi ya Jose Mourinho kama meneja wa Inter Milan, mchezaji huyu alifaidika kutokana na ujuzi wa Benitez na jeraha la Diego Milito. Mchezaji huyo kutoka Argentina, alikuwa ndiye mshambulizi wa timu hiyo lakini Eto'o ameonyesha kuwa anaweza kushikilia nafasi hiyo.

Eto'o anashikilia nafasi ya kwanza katika idadi ya mabao ya klabu bingwa barani ulaya, akiwa ameweza kufunga mabao saba katika mechi nne tu. Lakini kimataifa , mchezaji huyo kutoka Cameroon hajakuwa na mwaka mzuri.

Timu yake ya taifa ya Cameroon, Indomitable Lions, haikucheza vyema katika kombe la dunia na pia kwenye kombe la taifa bingwa barani Afrika. Hata hivyo Eto'o aliweza kufunga mabao manne katika mechi saba huko Angola na Afrika Kusini.

Umahiri wake katika mechi za klabu yake ulimuwezesha Eto'o kuwa kati ya wale wachezaji waliowania taji la FIFA la mchezaji bora duniani mwaka wa 2010.

SAMUEL ETO'O MAONI YA WATAALAM

Image caption Samuel Eto'o

Samuel Eto'o anafaa kushinda taji la mwanasoka bora wa Afrika wa BBC kwa kuwa licha ya kuwa miongoni mwa wachezaji bora, si Afrika tu bali pia duniani, hajawahi kutuzwa.

Mnamo mwezi wa Mei, Eto'o alikuwa mchezaji wa kwanza kushinda mashindano matatu mfululizo, alipoisaidia timu yake ya Inter milan kushinda taji la klabu bingwa barani Ulaya na ligi ya italia. Alipata mafanikio haya pia akiichezea timu ya Barcelona.

Cha muhimu ni kuwa mchezaji huyu hakucheza nafasi yake ya kawaida lakini hata hivyo alicheza kwa ustadi mkubwa.

Chini ya kocha Benitez, mchezaji huyu ameikumbusha dunia ustadi wake katika soka. Katika michezo 13 katika Serie A na klabu bingwa barani ulaya, tayari alikuwa amefunga mabao 14 wakati ambapo uchambuzi huu unafanywa.

Hali ya kutoridhisha ya timu ya Cameroon ndiyo sababu inayomzuia Eto'o kulishinda taji hili. Lakini je, ni kosa lake kuwa timu ya nchi yake imeshindwa mara tano katika mashindano saba ?