Chelsea yakataa kushindwa nyumbani

Aston Villa
Image caption Wachezaji wa Villa wakifurahia sare ya 3-3

Bao la Ciaran Clark muda wa majeruhi uliiwezesha Aston Villa kuondoka angalau na pointi moja katika uwanja wa Stamford Bridge, baada ya kusawazisha na kutoka sare ya magoli 3-3 dhidi ya wenyeji Chelsea, katika mechi iliyochezwa siku ya Jumapili.

Chelsea walikuwa wanaongoza, kufuatia Florent Malouda kuchezewa vibaya, na Frank Lampard kufunga bao la penalti, kabla ya Ashley Young naye kupata penalti ya kuiwezesha Villa kusawazisha.

Lakini sare hiyo haikuwa ya muda mrefu, kwani Emile Heskey alitia wavuni bao la kichwa, na Villa kuongoza kwa magoli 2-1.

Furaha ya Villa nayo haikudumu pia, kwani Didier Drogba aliweza kufunga bao la kusawazisha, na nahodha John Terry pasipo huruma akatia wavuni bao, na matokeo kuwa 3-2.

Licha ya kuchezea uwanja wa nyumbani, na kushangiliwa mno na mashabiki wa nyumbani, Villa walijizatiti na Clark aliweza kufunga kwa kichwa mpira aliopitishiwa na mchezaji mwenzake, Marc Albrighton.

Mchezo wa pili wa ligi kuu ya Premier jana ulikuwa ni kati ya Wigan na Newcastle, na ambao ulikwisha kwa ushindi wa wageni, 1-0.

Shola Ameobi, akicheza mahala pa Andy Carroll ambaye anaugua, aliweza kupata bao kipindi cha kwanza, katika dakika ya 19, baada ya awali Ali Al Habsi kuzuia mkwaju wa Joey Barton, na Peter Lovenkrands kugonga mwamba.

Wageni Newcastle, kupitia Fabricio Coloccini, awali pia walikuwa wamegonga mwamba.

Jumapili nchini Uskochi pia kulikuwa na msisimko mkubwa, wakati Georgios Samaras alipofunga mara mbili na kuiwezesha Celtic kuwafunga wenyeji Rangers magoli 2-0.

Image caption Wachezaji wa Celtic

Celtic sasa wamewaacha wapinzani wao wa karibu sana, Rangers, kwa pointi nne katika ligi kuu ya Uskochi.

Rangers walizuiwa kupata bao la mapema katika dakika ya tano, baada ya Emilio Izaguirre kuuelekeza mpira wa kichwa juu ya goli.

Celtic hatimaye waliweza kuthibitisha maarifa yao, wakati Samaras alipomzunguka kipa Allan McGregor, na kufunga bao la kwanza katika dakika ya 62.

Bao la pili lilifuata dakika nane baadaye, wakati Samaras alipoangushwa na Madjid Bougherra, na kufunga kwa mkwaju wa penalti.