Barmasai ashinda Dubai Marathon

David Barmasai Tumo
Image caption Barmasai ni bingwa wa Dubai Marathon

Mwanariadha wa Kenya, David Barmasai siku ya Ijumaa aliibuka bingwa wa mbio za Dubai Marathon, baada ya kujiandikishia muda wake bora zaidi katika mashindano hayo, saa 2, dakika 7 na sekunde 18.

Hii ni mara ya tatu mfululizo kwa mwanariadha huyo, mwenye umri wa miaka 22, kupata ushindi.

Mwaka jana Barmasai alikuwa ni mshindi wa mbio za marathon za Nairobi.

Akizungumza kwa Kiingereza na mwandishi wa BBC Andy Edwards, Barmasai alielezea kwamba mashindano hayo yalikuwa magumu mno, na hakutazamia kuwa mshindi.

"Kwa kweli ilikuwa vigumu mno kushinda mashindano haya. Sikufikiria ningeliweza kupata ushindi katika mashindano haya. Nimefurahi sana kuwatangulia wanariadha wote. Nilishangazwa sana wakati Eliud Kiptanui aliposhindwa kuendelea baada ya kilomita 30", alielezea Barmasai.

Barmasai amesema sasa anafikiria kujiandaa vyema kwa mashindano ya Tokyo Marathon nchini Japan, na kujaribu kuimarisha muda wake.

Mkenya Evans Cheruiyot alimaliza katika nafasi ya pili, na Eshetu Wendimu wa Ethiopia katika nafasi ya tatu.

Kwa upande wa kina dada, Aselefech Medessa wa Ethiopia alikuwa mshindi, kwa kumaliza katika muda wa saa 2, dakika 22, na sekunde 45, sekunde tatu tu kufikia muda bora zaidi wa mashindano hayo.

Lydia Cheromei wa Kenya alikuwa wa pili, na Isabella Andersson kutoka Sweden akamaliza katika nafasi ya tatu.