Djokovic ndiye bingwa Australia

Novak Djokovic amefanikiwa kumshinda Mwingereza Andy Murray katika fainali ya michuano ya wazi wa Australia, na kuzima kabisa matumaini ya Murray kunyakua taji la kwanza la juu la mchezo huo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Djokovic aliangamiza matumaini ya Uingereza kushinda baada ya miaka 75

Djokovic, raia wa Serbia mwenye umri wa miaka 23, alishinda kwa seti 6-4, 6-2, 6-3 na kujitwisha taji hilo alilolichukua kwa mara ya kwanza mwaka 2008.

Murray alikuwa na matumaini ya kuwa Mwingereza wa kwanza kuchukua taji la juu kama hilo, tangu mchezaji tennis Fred Perry wa Uingereza ashinde michuano ya wazi ya Marekani mwaka 1936.

Djokovic, anayeshika nafasi ya tatu katika msimamo wa wachezaji bora duniani aliingia katika fainali baada ya kumshinda bingwa mtetezi Roger Federer katika nusu fainali.

Akizungumza baada ya mchezo, Andy Murray ambaye ni mchezaji namba tano duniani amempongeza Djokovic kwa ushindi huo akisema alistahili, na kusema bila shaka watakutana siku nyingine katika mpambano kama huo.

Naye Novak Djokovic ambaye ametunuku ushindi wake huu kwa nchi yake amempongeza Murray, na kusema zilikuwa wiki mbili za kuvutia, na kwamba ulikuwa mchezo mgumu kwa sababau wanafahamiana kwa muda mrefu.

Mbali na kutunukia tuzo hiyo kwa nchi yake Serbia, Djokovic pia amewakumbuka waatirika wa mafuruko yaliyotokea nchini Australia.

Kwa upande wa wanawake, Kim Clijsters wa Ubelgiji aliibuka mshindi wa michuano hiyo ya wazi, baada ya kumshinda Li Na kutoka Uchina.