Canada yaishinda Kenya

Jimmy Kamande
Image caption Nahodha Kamande alisikitishwa na mchezo dhidi ya Canada

Matatizo ya Kenya katika mashindano ya Kombe la Dunia ya kriketi yaliendelea katika uwanja wa Feroz Shah Kotla mjini Delhi, India, wakati waliposhindwa na Canada, Jumatatu tarehe 7 Machi.

Huu ulikuwa ni ushindi wa pili kwa Canada, katika pambano la Kombe la Dunia, na ushindi wa kwanza, katika mashindano ya mwaka huu.

Canada ilinufaika sana kutokana na mchezaji Jimmy Hansra, ambaye aliweza kupata mikimbio 70, kikiwa ndio kiwango chake cha juu zaidi, kati ya mapambano 11 ya mechi za siku moja za kimataifa.

Aliisaidia Canada kupata jumla ya mikimbio 199, huku Wakenya wakipata 198.

Mchezaji huyo wa Canada aliyezaliwa India, alifanya juhudi kubwa, sawa na nahodha Ashish Bagai, katika kuiwezesha nchi yake kupata ushindi.

Nahodha wa Kenya, Jimmy Kamande, kwa masikitiko makubwa alisema: "Tulianza vibaya, vibaya sana, na nilidhani baadaye tulizinduka vyema".

Alielezea kwamba kuna wakati alidhani wataweza kupata kati ya mikimbio 220 hadi 230.

Kabla ya ushindi huo, mara ya mwisho Canada ilipata ushindi katika pambano la Kombe la Dunia mjini Durban, mwaka 2003, wakati ilipoishinda Bangladesh.