Kenya yabanwa na Australia

Australia, mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia la Kriketi, wamefanikiwa kuwa miongoni mwa mataifa manane yaliyofuzu kuingia robo fainali.

Image caption Walicheza kwa ushujaa lakini waliondolewa na Australia

Hata hivyo, Jumapili iliwabidi kupambana vikali na Wakenya, na hatimaye kupata ushindi kwa mikimbio 60.

Michael Clarke aliweza kupata mikimbio 93 na mwenzake Mike Hussey 54, na wakafanikiwa kuiokoa timu yao, kwa kupata jumla ya runs 324, huku Kenya ikipata 264.

Kufuatia kushindwa katika mapambano manne mfululizo, ilikuwa wazi Wakenya hawakutaka kuondolewa na Australia pasipo kuonyesha kikamilifu kwamba wanaumudu mchezo wa kriketi.

Tanmay Mishra alifanikiwa kupata runs 72, huku Collins Obuya akipata 98, na pasipo kuondolewa.

Thomas Odoyo aliweza kuungana na Wakenya wenzake katika kuitisha timu hiyo ya Australia, lakini hatimaye timu ya Australia ilithibitisha ndio bora, na kupata ushindi.

Kenya itacheza na Zimbabwe tarehe 20 mwezi Machi.