Wote lazima kushirikishwa kabla ya kubadilisha ratiba

Mkuu wa mashindano ya Formula 1, Bernie Ecclestone, ametangaza kwamba makala ya Bahrain ya mashindano ya magari ya Grand Prix hayatafanyika mwezi Oktoba kama ilivyopangwa, baada ya awali kuahirishwa.

Mashindano hayo yalitazamiwa kuufungua msimu huu mwezi Machi, lakini yakaahirishwa kutokana na vurugu za kisiasa nchini humo.

Wiki iliyopita, chama cha mashindano ya magari cha FIA kilitangaza kuyarudisha mashindano ya Bahrain katika kalenda ya msimu huu.

"Matazamio ni kwamba itawezekana mashindano kufanyika, lakini kwa hakika, hayapo bado", Ecclestone alimuelezea mwandishi wa BBC wa michezo, Dan Roan.

Image caption Asema timu lazima kushauriana kubadilisha kalenda

"Ratiba ya mashindano haiwezi kupangwa upya pasipo kuwashirikisha wahusika".

Maoni ya Ecclestone yamejitokeza baada ya timu moja, kati ya 12, kukataa kuidhinisha mabadiliko hayo.

Mashindano ya Bahrain yaliondolewa katika ratiba mwezi Februari kutokana na maandamano kutaka mabadiliko ya kisiasa, na wakati watu 20 waliuawa.

Hata hivyo, chama cha FIA kiliamua kuyarudisha mashindano ya Bahrain baada ya kupokea ripoti kwamba mambo sasa yametulia.

Rais wa kamati ya kimataifa ya uongozi wa mchezo huo, Jean Todt, ameielezea BBC kwamba FIA iliamua kwa pamoja kuunga mkono uamuzi wa mashindano ya Bahrain kufanyika, baada ya kushauriana na makamu-rais wa chama, Carlos Gracia.

"Mjumbe wetu maalum alikuwa na vikao vingi nchini Bahrain, ikiwa pia ni pamoja na kukutana na watu waliohusika katika masuala ya haki za kibinadamu", alielezea Todt.

"Alikuta hali imetulia, hali ya utulivu, na kwa pamoja tukakata kauli".

Bahrain ilikabidhiwa nafasi ya India, tarehe 30 mwezi Oktoba, katika kalenda yenye mashindano 20, huku India, ikitazamia kuwa mwenyeji wa mashindano yake ya kwanza, ikishauriwa kwamba yamesogezwa mbele hadi tarehe 11 Desemba.