Chama cha soka cha Misri kimeamua kuachana na kocha wa timu ya taifa Hassan Shehata baada ya pande zote mbili kushauriana

Chama cha soka cha Misri, leo kimeitisha kikao cha dharura kumjadili kocha wa timu ya taifa, Hassan Shehata, na baada ya pande zote mbili kushauriana, amekubali kujiuzulu.

Shehata, mwenye umri wa miaka 61, ndiye kocha aliyefanikiwa sana katika historia ya kuiongoza timu ya Firauni (Pharaohs), na ambayo imetwaa ubingwa wa fainali tatu za michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika iliyopita.

Image caption Chama cha soka Misri kimemuachisha kazi

Lakini Shehata alizidiwa kikazi, kwani timu ya Misri, katika kundi la G, haikuonyesha mchezo wa kuwaridhisha mashabiki, katika mechi za kufuzu kwa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2012.

Sasa chama cha soka cha Misri kimeamua hakiwezi tena kuendelea kupokea huduma zake.

Sare ya Jumapili ya 0-0 dhidi ya Afrika Kusini imewafanya mabingwa watetezi kushikilia nafasi ya mwisho katika kundi hilo la G, na pasipo kupata ushindi katika mechi nne zilizopita.

Timu ya Misri ilihitaji kupata ushindi katika mechi ya Jumapili mjini Cairo, ili kuwa katika nafasi nzuri ya kujitengea nafasi kulitetea kombe katika mashindano yatakayofanyika kwa ushirikiano wa Equatorial Guinea na Gabon.

Kutokana na mechi hiyo ambayo haikuwa na magoli, hasa kutokana na juhudi za walinda lango, matumaini ya Misri ya kufika katika mashindano ya Januari yametokomea.

Wamisri, ambao walikuwa mabingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2006, 2008 na 2010, walifanikiwa kufunga goli mara moja tu katika jumla ya saa sita za timu hiyo kupambana uwanjani.

Kampeni yao ya kufuzu kwa mashindano hayo ilianza kwa kusuasua, wakati ilipotoka sara na Sierra Leone katika mechi ya nyumbani mjini Cairo, na timu hiyo ya Firauni ilistajabishwa hata zaidi kwa kuzabwa bao 1-0 na Niger.