Mwenge wa Olimpiki wazinduliwa mjini London

Olimpiki 2012
Image caption Michezo ya London

Mwenge wa mashindano ya Olimpiki ya mwaka 2012 mjini London umezinduliwa ukiwa ni wenye pembe tatu zenye rangi ya dhahabu inayomeremeta.

Mwenge huu uliotengenezwa na kampuni kutoka eneo la mashariki mwa jiji umetengenezwa kwa matundu ingawa umeundwa kwa mchanganyiko wa alumiamu na kupakwa dhahbu.

Kutokana na madini yaliyotumiwa pamoja na ustaadi uliotumiwa mwenge huu utakuwa mwepesi kiasi kwamba vijana 8,000 watakaoubeba kupitia mitaa ya London hawatochoshwa wala kuudondosha.

Sherehe ya kuubeba ya siku 70 itazunguka kote nchini Uingereza na kutimiza maili 8,000 kabla ya kuwasili mahali yatakapofanywa mashindano.

Mzunguko huo wa kupokezana mwenge utaanza tarehe 19 May kabla ya kurudi kwenye uwanja wa Olimpiki mjini Stratford tayari kwa sherehe ya kuukoka moto siku ambapo sherehe za ufunguzi wa mashindano zitafanywa tarehe 27 Julai mwaka 2012.

Shughuli ya kuchagua watu mashuhuri wenye ushawishi miongoni mwa Waingereza wengi wao wakiwa wenye umri ulio kati ya miaka 12 -24 kuubeba mwenge huo imeanza.

Asili ya kupokezana Mwenge Asili ya kupokezana mwenge ni huko Ugiriki, ambako wajumbe walitumwa kutoka mji wa Olimpia kutangaza tarehe za mashindano na vilevile kutoa witowa kukomesha vita vya aina yoyote wakati michezo ikifanyika.

Hali hiyo ilibadilika kuambatana na nyakati kunako michezo ya Olimpiki mjini Berlin mwaka 1936, na tangu hapo shughuli hii imebadilika na kuwa sherehe ya kufana kama chachu ya kifungua michezo.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption hubadilika kila michezo

Muundo wa mwenge umebadilika kwa kila mashindano, mara kwa mara ukionyesha ubora wa muundo, na mara nyingi ukimulika hali ya wakati.

Kwa mashindano ya kisasa ya Olimpiki, moto huashwa huko Olympia yalikoanzia mashindano haya kwa kutumia miyale ya Jua na kuzunguka kote nchini Ugiriki.

Tofauti na desturi iliyokuepo, mwenge wa mashindano ya mwaka 2012 hautozunguka dunia bali shughuli hiyo itafanywa hapa Uingereza.