Semenya kutokwa kijasho tena!

Image caption Caster Semenya

Bingwa wa mbio za Mita 800 kwa wanawake Caster Semenya kutoka Afrika Kusini, anakabiliwa na kibarua kigumu kudhihirisha umahiri wake katika riadha leo jioni wakati atakapokutana uso kwa macho na nyota wengine katika mbio hizo wakati wa Mashindano ya riadha ya Diamond League nchini Norway.

Semenya hakuweza kurindima katika mashindano ya Diamond League mjini Eugine, jimbo la Oregon nchini Marekani jumamosi iliyopita, baada ya kushindwa na Kenia Sinclair wa Jamaica. Semenya alikamata nafasi ya pili huku Janeth Jepkosgei wa Kenya akikamilisha katika nafasi ya tatu.

Mashindano ya dunia

Kwa mara nyingine mashindano hayo yanatarajiwa kushuhudia msisimko wa aina yake wakati jogoo wa mbio za mita mia moja kwa wanaume, Usain Bolt kutoka Jamaica akishiriki katika mashindano ya mbio za mita 200 kwa mara ya kwanza katika kipindi cha mwaka mmoja.

Wengi wanariadha hao wanatumia mashindano hayo ya Diamond League kujiandaa kwa mashindano ya ubingwa wa riadha duniani yatakayoandaaliwa nchini Korea Kusini baadaye mwaka huu.