Tiger Woods ajiondoa US Open

woods Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Tangu mwaka wa 2009 Woods angali anachechemea

Mchezaji wa gofu wa Marekani Tiger Woods hatashiriki mashindano ya US Open kuanzia Juni tarehe 16 hadi 19 kwa sababu ya jeraha la mguu wa kushoto.

Woods, ambaye alishikilia nafasi ya kwanza duniani kwa muda mrefu, alipata jeraha hilo katika raundi ya tatu ya Masters mwezi Aprili.

``Nimeudhika sana sitacheza US Open,'' Woods alinukuliwa akisema kwenye mtandao.

``Ni mhimu nitilie maanani wanayoniambia madaktari wangu kwa manufaa yangu mwenyewe. Nilikuwa natarajia nitashiriki mashindano hayo lakini haingewezekana kwa sababu ningeumia zaidi.''

Tangu mwaka wa 2009 alipoibuka mshindi kwenye mashindano ya Australian Masters, Woods hajawahi kushinda tena kwenye mashindano 22.

Woods ameshiriki mashindano yote ya US Open tangu mwaka wa 1994 lakini kwa miaka mitatu iliyopita amekumbwa na majeraha. Taji lake kuu la mwisho aliloshinda ni mwaka wa 2008 la US Open alipomuondoa Rocco Mediate.