Andy Murray wa Uingereza amesema hana utani na mpinzani Daniel Gimeno-Traver

Andy Murray amepuuza uwezekano wa kucheza na mchezaji bora zaidi duniani, Rafael Nadal, katika nusu fainali ya Wimbledon, akisema muhimu kwanza ni kuangazia pambano lake la raundi ya kwanza.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Hamna haja ya kufikiria pambano la nusu fainali dhidi ya Nadal pasipo kufikiria raundi ya kwanza ya Wimbledon

Murray, ambaye amepangwa katika mapambano hayo kucheza dhidi ya Nadal katika wachezaji wanne wa mwisho watakaosalia, amesema muhimu zaidi hivi sasa ni kufikiria namna atamshinda Daniel Gimeno-Traver kutoka Uhispani katika raundi ya kwanza.

Baada ya Roger Federer kutolewa jasho na Alejandro Falla mwaka jana katika raundi ya kwanza, Murray, mwenye umri wa miaka 24, kamwe hataki kufanya mzaha katika mashindano hayo.

Alisema: "Haina haja ya kumfikiria Rafa katika nusu-fainali, muhimu ni kulifikiria pambano la kwanza."

Federer mwaka jana alihitaji kucheza seti tano ili kumshinda Falla, na Murray hana matazamio ya mchezo rahisi dhidi ya Gimeno-Traver, ambaye katika orodha ya wachezaji bora ulimwenguni, amepangwa katika nafasi ya 56.

Mchezaji huyo wa Uskochi aliibuka bingwa katika mashindano ya Uingereza ya Queen's Jumatatu iliyopita, lakini ataingia pambano la Wimbledon akihisi kana kwamba amepungukiwa kwa kutofanya mazoezi ya kutosha, baada ya mvua kutatiza pambano la kuonyesha uhodari wake dhidi ya Viktor Troicki, kutoka Serbia, kukatizwa kwa mvua siku ya Ijumaa.

Alikuwa akiongoza 4-1 wakati pambano hilo la Boodles Challenge, katika uwanja wa Stoke Park, Buckinghamshire, kusimamishwa.

Katika mashindano ya Wimbledon, Andy Murray amepangwa katika nafasi ya nne, baada ya Nadal, Djokovic na Federer.