FIFA ingali kimya kuhusu uchaguzi Kenya

Kamishena wa michezo nchini Kenya Gordon Oluoch amesema shirikisho linalosimamia kandanda duniani, Fifa, lingali kimya kuhusu kugharamia uchaguzi huo ambao sasa utafanyika Agosti tarehe 13 mwaka huu.

Kulingana na Oluoch bodi inayoandaa uchaguzi huo, Independent Electoral Board (IEB) inahitaji kama dola 550,000 kuandaa uchaguzi mkuu wa kandanda nchini Kenya lakini kufikia sasa Oluoch anasema Fifa imetoa dola 44,000.

``Tunaomba Fifa itimize ahadi yake ya awali ya kugharamia uchaguzi wa Kenya kwa sababu sisi kama serikali hatuwezi. Kwanza hizo fedha haziko kwenye bajeti yetu na pili kugharamia uchaguzi itakuwa tunakiuka taratibu za Fifa za serikali kutojihusisha na usimamizi wa kandanda,'' alisema Oluoch, na kuongeza:``Huu ndio wakati muafaka Fifa ionyeshe kweli inanuia kuendeleza kandanda nchini Kenya kama inavyosema mara kwa mara.

Mbali na fedha, tatizo jingine linalokumba IEB ni kupata idadi ya vilabu kamili vinavyoshiriki ligi za daraja la chini kwani kwa mara ya kwanza katika uchaguzi mkuu wa kandanda nchini Kenya ni vilabu ndivyo vitakavyochagua mwenyekiti na wasaidizi wake, na wajumbe kama ilivyokuwa miaka iliyopita.

Kulingana na Oluoch ligi kadhaa hazina kumbukumbu za mechi zao hivyo basi inakuwa vigumu kujua ni vilabu gani vitakavyoshiriki uchaguzi huo.

``Sisi hatuhusiki na shughuli hiyo ya vilabu. Fifa imesema hilo sio jukumu letu na tukifanya hivyo tutakuwa tunakiuka taratibu zao kwa hivyo tumeachia FKL na KFF ziwasilishe idadi yao ya vilabu vilivyo chini yao,'' alisema Oluoch.

Miongoni mwa wanaogombea uenyekiti ni kinara wa FKL Mohammed Hatimy, mkuu wa KFF Sam Nyamweya, naibu wake Twaha Mbarak, Mohammed Hussein na mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Kenya Harambee Stars Sammy Shollei. Katibu wa baraza linalosimamia vilabu vya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) Nicholas Musonye naye yuko mbioni lakini hajatangaza rasmi kama atagombea uenyekiti.