Tanzania tayari kuandaa kindumbwendumbwe

 Mashindano ya Cecafa
Image caption Mashindano ya Cecafa

Jumla ya timu 12 zitashiriki katika mashindano ya kandanda ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati ambayo yanaanza Jumamosi wiki hii jijini Dar es Salaam na Morogoro, Tanzania.

Droo imefanyika Jumanne wiki hii mjini Nairobi na mechi za ufunguzi ni Etincelles ya Rwanda dhidi ya Ocean Boys ya Zanzibar kuanzia saa nane za mchana kisha saa kumi Simba ya Tanzania inadundadunda uwanjani na Vital'0 ya Burundi zote zikiwa ni mechi za kundi la A.

Timu zilizoko kundi B ni Yanga ya Tanzania, El Merreikh ya Sudan, Bunamwaya kutoka Uganda na Elman ya Somalia. Mechi za makundi hayo zitafanyika katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam na za kundi la C zitachezewa Morogoro. Timu zilizoko kundi hilo ni bingwa mtetezi APR ya Rwanda, St George kutoka Ethiopia, Ulinzi ya Kenya na Ports ya Sudan.

Katibu wa baraza linalosimamia vilabu vya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) Nicholas Musonye amesema Rais wa Rwanda Paul Kagame kama kawaida yake atatoa dola 60,000 na Tanzania Breweries dola 100,000 za kudhamini mashindano haya ya kila mwaka.

``Tumekubaliana pia na televisheni ya Afrika Kusini Supersport kuonyesha mechi hizo moja kwa moja na kuna mdhamini wa Sudan ambaye amelipia timu zote usafiri,'' anasema Musonye.

Bingwa mtetezi APR itaingia uwanjani Juni tarehe 26 kwa mechi ya ufunguzi dhidi ya Ports ya Djibouti kuanzia saa kumi na mjini Dar es Salaam Yanga inakwaruzana na El Merreikh kuanzia saa kumi pia..