16 wachuana kupiga hatua Wimbledon

Wanaume 16 hapo kesho wataingia ukumbi wa Wimbledon kwa matarajio ya kufuzu kwa robo fainali ya mashindano haya.

Haki miliki ya picha getty
Image caption Bingwa mtetezi Rafael Nadal

Mmoja wa wachezaji hao wa Tennis ni mpya kabisa akijiweka katikati ya miamba ya mchezo wa Tennis naye ni wa Australia. Mbali na Tomic wengine waliofuzu ni nyota wa mchezo huu Rafael Nadal, Roger Federer, Novak Djokovic na Andy Murray.

Tomic ni mchezaji ambaye wengi wanahisi ni mrithi wa nyota wa zamani wa Australia Mark Philipousis na Leyton Hewit.

Kufikia hatua hii ya kulenga robo fainali Tomic alimbwaga mwamba mwingine Robin Soderling katika seti tano jumamosi.

Kabla ya pambano hilo Soderling alimuondoa Leyton Hewit na labda Tomic alilipiza kisasi na kujifunza machache kutoka kwa nyota wa Australia.

Na kesho jumatatu Tomic atachuana na Xavierr Malisse wa Ubelgiji.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Uwanja wa Wimbledon

Ufanisi wa kijana Tomic umeelezewa na Roger Federer kama mwamko wa kizazi kipya katika tennis na ishara nzuri kwa mchezo wa Tennis kwa ujumla.

Kwa upande wake Federer anatazamia hatua moja kabla ya kufikia fainali ya mara tisa uwanja wa Wimbledon na ushindi wake wa mara ya saba atakapopambana na Mikhail Youzhny.

Andy Murray wa Uingereza atachuana na Richard Gasquet wa Ufaransa. Mfaransa mwingine katika mchanganyiko huu ni Michael Llodra ambaye atachuana na mchezaji ambaye kwa kipindi cha mwaka mzima amepoteza mechi moja kati ya 45 Novak Djokovic. Wengine ni Tomas Berdych aliyefika fainali ya mwaka jana akitifua vumbi na Mardy Fish, Lukasz Kubot apambane na Feliciano Lopez wakati David Ferrer akitoana jasho na Jo-Wilfried Tsonga.

Kwa upande wa wanawake Serena Williams anajitahidi kufikia rekodi ya Steffi Graf, mwanamke wa mwisho kushinda hapa Wimbledon mara tatu mtawalio. Serena ambaye ameshinda mara nne hapa Wimbledon alifuzu kwa kumtwanga Maria Kirilenko 6-3 6-2.Serena atachuana na Marion Bartoli.

Bingwa wa mwaka 2004 wa Wimbledon Maria Sharapova alimshinda Klara Zakopalova 6-2.6-3 katika mchuano uliokuwa mgumu na kesho anatazamiwa kuzipiga na Shuai Peng wa Uchina.