Ashley Young kujiunga na Man United

Ashley Young
Image caption Ashley Young kuhamia Man United

Mchezaji wa Aston Villa Ashley Young anatarajiwa kujiunga na Manchester United.

BBC imepata taarifa kuwa mchezaji huyo wa timu ya taifa ya England mwenye umri wa miaka 25 yuko karibu kwenda Old Trafford kwa kitita cha pauni za Uingereza milioni £17m.

Amekuwa na timu hiyo ya Aston Villa kwa muda wa miaka minne na nusu akitokea timu ya Watford na alikuwa amebaki na mwaka mmoja kabla ya kukamilisha kandarasi yake na Villa.

Young - ambaye hivi majuzi aliifungia England wakati walipotoka sare ya magoli 2-2 na Switzerland -amechezea timu yake ya taifa mara 15.

McLeish alikiri Young ataondoka

Kocha mpya wa Villa Alex McLeish alikiri mapema wiki hii kuwa Young alitarajiwa kuondoka msimu huu.

" Haijathibitishwa kwa sasa lakini inaonekana anaondoka,"McLeish aliambia talkSPORT.

" Kwa maoni yangu itakuwa vigumu kumzuia asiondoke."

Haki miliki ya picha Other
Image caption Alex McLeish

Iliwagharimu Villa pauni za Uingereza milioni 9.65 kumpata Young Januari mwaka 2007 na ameifungia timu hiyo magoli 30 katika ligi kuu ya Uingereza.

Mchezaji wa Manchester United Michael Owen alisema kwenye mtandao wa twitter: " Naona Ashley Young amefanyiwa uchunguzi wa matibabu.Natarajia kuwa kila kitu kitakuwa sawa kwa kuwa atakuwa mchezaji mzuri kwetu."

Kocha wa Manchester United Sir Alex Ferguson amempoteza mchezaji wa muda mrefu Paul Scholes ambaye amestaafu mapema mwezi huu na tayari ameshamchukua kijana wa Blackburn Phil Jones kuchukua nafasi ya Scholes.

Sir Alex Ferguson pia anatafuta golikipa mwengine atakayechukua nafasi ya Edwin van der Sar ambaye amestaafu.