Dereva wa Uganda Posiano Lwakataka ameibuka bingwa wa mashindano ya magari Pearl of Africa

Dereva wa nyumbani Posiano Lwakataka ameibuka bingwa wa mashindano ya magari ya ubingwa wa Afrika, Pearl of Africa, mwaka 2011 na ya 14, yaliyomalizika Jumapili mjini Kampala Uganda.

Image caption Lwakataka ameibuka bingwa wa mashindano ya magari ya Pearl of Africa

Mashindano yalianza siku ya Ijumaa yakizunguka wilaya za mashariki mwa Uganda, kukiwa na magari 28, na yaliyomaliza mashindano ni magari 16.

Posiano Lwakataka wa Uganda akiendesha gari aina ya Subaru Impreza alimaliza mashindano ya mwaka huu ya kilomita 609.44 kwa kumaliza kwa muda wa saa 2:03.42.

Aliyechukua nafasi ya pili ni Fiditisi Chrstakies kutoka Rwanda.

Alimaliza kwa muda wa saa 2:13:45.

Mwanadada pekee aliyeonyesha ushujaa kutwaa ubingwa wa kitaifa ni Susan Mwonge wa Uganda, aliyemaliza katika nafasi ya nne kwa muda wa saa 2:14:32.

Image caption Dereva wa kike Uganda aliyemaliza katika nafasi ya nne

Susan anasema anataka kuandika historia ya mbio za magari nchini Uganda kutwaa ubingwa wa kitaifa.

Aliyekuwa bingwa wa mwaka jana Jime White kutoka nchini Zimbabwe hakuweza kumaliza baada ya gari lake kupata matatizo ya 'gearbox' leo asubuhi kama anavyosema mwenyewe:

Alielezea gari lilikuwa na matatizo ya 'gearbox' baada ya kumaliza sehemu ya kwanza, akielekea ya pili, lakini hakuweza kumaliza, ila alikuwa na matumaini makubwa kupata pointi katika mashindano hayo, kama angemaliza na kuongeza pointi kuwania ubingwa wa Afrika.

Lakini sasa anaangazia mashindao yaliyobaki matatu.

Dereva mwingine aliyeondoka katika mashindano baada ya kuongoza siku ya kwanza na ya pili ni Jas Mangat wa Kenya, ambaye gari lake lilipata matatizo na kushindwa kumaliza.