Manchester City kumsajili Sergio Aguero

Image caption Sergio Aguero

Mshambuliaji wa Argentina Sergio Aguero amewasili mjini Manchester kukamilisha kuhamia kwake Manchester City baada ya kukubaliana juu ya malipo na Atletico Madrid.

Inasemekana kuwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 amekubali kandarasi ya miaka mitano, kwa kiasi cha pauni za Uingereza milioni £38m.

Katika mtandao wa Tweeter Aguero alisema: " Mimi tayari ni mchezaji wa Man City. Nimefurahi kuwa na timu kuwa mji huu."

Man City waliendelea na juhudi zao za kumsajili Aguero licha ya mpango wa Carlos Tevez kuhamia Corinthians kutibuka.

Mshambuliaji huyo,anayejulikana kwa jina la utani kama 'Kun', alihusishwa pia na Real Madrid na Juventus lakini atakuwa mchezaji wa gharama ya juu zaidi kuwahi kusajiliwa na Manchester City, amemshinda Robinho aliyesajiliwa kwa pauni za Uingereza milioni £32.5m mwaka 2008.

Aguero aliwasili nchini Uingereza kutoka Buenos Aires,Jumatano asubuhi na kwenda moja kwa moja katika hospitali moja ya kibinafsi mjini Manchester kufanyiwa uchunguzi wa matibabu.

Baadaye jioni alifika katika uwanja wa Manchester City, na baada ya kufanya mazungumzo na maafisa wa timu hiyo, alisalimiana na mashabiki wengi waliokuwa wamefika katika uwanja huo kumuona.