Bingwa wa dunia Usain Bolt aliondolewa katika fainaili za mita 100 mashindano ya dunia mjini Daegu baada ya kuanza mbio mapema, huku raia mwenzake wa Jamaica Yohan Blake akinyakua medali ya dhahabu.

Usain Bolt Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Afunika uso kwa kupigwa butwaa kwa yaliyompata

Mwanariadha wa Jamaica Usain Bolt aliondolewa katika fainali za mita 100 kwa wanaume katika mashindano ya dunia ya riadha ya Daegu, Korea ya Kusini, huku raia mwenzake wa Jamaica, Yohan Blake, akipata dhahabu.

Bingwa mtetezi Bolt aliwashangaza mashabiki wengi wa riadha katika uwanja wa Daegu, alipoondolewa kwa kuanza mbio hata kabla kusikia mlio wa bunduki.

Blake aliweza kukamilisha mbio hizo kwa sekunde 9.92, akimtangulia Mmarekani Walter Dix (10.08) na bingwa wa dunia mwaka 2003, Kim Collins (10.09).

Lakini gumzo hasa ambalo linaendelea ni kumhusu Bolt, ambaye bado alitazamiwa kushiriki katika mbio za mita 200m na 4x100.

Kabla ya mbio, kama kawaida, Bolt alionekana kutulia.

Wengi watajiuliza ikiwa yaliyompata Bolt ni kufuatia sheria mpya kuanzishwa, inayohusu kuanza mbio mapema kabla mlio wa bunduki.

Kanuni hiyo ya riadha, nambari 162.7, inaelezea kwamba ikiwa mwanariadha ataanza mbio mapema kabla ya mlio huo, basi ataondolewa katika mashindano.

Kitambo, mwanariadha alisamehewa alipofanya kosa hilo mara ya kwanza, na aliondolewa katika mashindano iwapo alirudia kosa hilo mara ya pili.

Sheria hiyo mpya ilitangazwa na shirikisho la kimataifa la riadha, IAAF, mwanzoni mwa msimu wa riadha mwaka 2010.

Ijapokuwa Blake, mwenye umri wa miaka 21 alimsikitikia mwenzake Bolt, na ambaye hufanya mazoezi naye, alisema alifurahishwa sana na ushindi huo wa ghafula.

"Sidhani nina maneno ya kuelezea hayo, na ninahisi kulia machozi," alisema. "Nimekuwa nikisali kupata ushindi, na hii kwangu ni ndoto.

"Usain Bolt amekuwa akinisaida. Nilihisi nitapata ushindi kwa niaba ya Bolt."

Collins, mwenye umri wa miaka 35, na alielezea wasiwasi wake kuhusiana na sheria hiyo mpya, baada ya kupata medali yake ya shaba.

"Sidhani sheria hii ni sawa. Mambo haya hutokea na ni lazima uwape watu nafasi," alielezea mwanariadha huyo kutoka St Kitts na Nevis.

Bolt, mwenye umri wa miaka 25, amekuwa akiwika katika mbio fupi miaka michache iliyopita, tangu alipovuma na kuandikisha rekodi katika mbio za mita 100 na 200 katika mashindano ya Olimpiki 2008 na vile vile Roma, akiandikisha muda wa sekunde 9.58 na 19.19.

Baadhi ya wanariadha wazoefu wa mbio za mita 100 walikuwa wamekosekana katika fainali hizo za Daegu, ikiwa ni pamoja na wanariadha Asafa Powell, Steve Mullings, Tyson Gay na Muingereza Dwain Chambers ambaye aliondolewa katika nusu fainali, pia baada ya kuanza mbio kabla ya mlio wa bunduki.