Andy Murray ni kati ya wachezaji 16 waliosalia katika mashindano ya tennis ya US Open

Andy Murray alifuzu kwa urahisi kuwa miongoni mwa wachezaji 16 waliovuka mapambano ya mwanzomwanzo na kusalia katika mashindano ya tennis ya Marekani ya US Open.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Tangu alipofika fainali mwaka 2008 Andy Murray hajafanikiwa kuwa miongoni mwa wale wanaofuzu kucheza robo fainali katika mashindano ya New York

Mchezaji wa Uingereza Murray alimshinda Mhispania Feliciano Lopez.

Katika mapambano yao ya awali kabla kukutana katika mashindano ya Marekani, Murray alikuwa amemshinda mpinzani wake mara tano, ambaye amepangwa katika nafasi ya 26 miongoni mwa wachezaji bora zaidi wa kiume duniani.

Murray alipata ushindi wa 6-1 6-4 6-2.

Murray, mwenye umri wa miaka 24, alithibitisha kikamilifu kwamba alikuwa ni mchezaji bora zaidi kumshinda mpinzani wake katika pambano hilo la New York.

Sasa atacheza na Donald Young katika raundi ya nne, Jumanne.

Licha ya kupangwa katika nafasi ya 84 katika mashindano hayo, Murray amesema kamwe hawezi kumpuuza mpinzani wake Mmarekani Young, watakapopambana katika uwanja wa Flushing Meadows.

Young alimshangaza Murray alipomshinda katika mashindano ya India Wells mwezi Machi.

Naye bingwa mtetezi katika mashindano hayo, Rafael Nadal kutoka Uhispania, na aliyeanguka baada ya kupata na maumivu ya misuli akiwa katika mkutano na waandishi habari, mara tu baada ya kumshinda David Nalbandian kutoka Argentina, amesema ameweza kupata nafuu, na alielezea kwamba alizidiwa kutokana na joto kali.