Mchezaji bora zaidi wa Uingereza katika mchezo wa tennis na nambari 4 duniani Andy Murray asema kuna uwezekano wa wachezaji wa kulipwa kufanya mgomo ikiwa maslahi yao ya mabadiliko ya ratiba yatapuuzwa

Andy Murray Haki miliki ya picha Getty
Image caption Asema kuna uwezekano wa wachezaji tennis kufanya mgomo juu ya malalamiko ya ratiba

Andy Murray amesema wachezaji bora zaidi wa tennis ya kulipwa wangelipenda kuona mabadiliko katika ratiba ya mapambano yao, na kuna uwezekano wa kuyagomea mashindano ikiwa maslahi yao hayatatiliwa maanani.

Amesema wachezaji wengi wamekuwa wakiudhika mno kutokana na ratiba iliyosongamana, na watakutana mjini Shanghai mwezi ujao kujua hatua watakazoweza kuzingatia.

Murray ameielezea BBC kwamba kuna uwezekano wa mgomo kufanyika.

"Kuna uwezekano. Nafahamu hilo, kwani baada ya kuzungumza na baadhi ya wachezaji, wao hawana wasiwasi wa kufanya hivyo [kugoma].

"Tutumaini kwamba hatutafikia hatua hiyo, lakini nina hakika wachezaji wataifikiria."

Alipoulizwa ikiwa suala hilo la mgomo litajadiliwa nchini Uchina, alijibu: "Ndio, nafikiria hivyo".