Obua wa Cranes afukuzwa kambini

Obua
Image caption David Obua

Maandalizi ya timu ya taifa ya Uganda, The Cranes katika mchezo wa kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Kenya yameingia dosari baada ya David Obua kufukuzwa kambini.

Kiungo huyo awali aliondoka kambini baada ya kufahamu kuwa hatoruhusiwa kuuliza swali lolote wakati rais atakapozuru kambi yao.

Rais Yoweri Museveni alitembelea kambi ya Cranes Ijumaa Asubuhi ili kujenga morali ya kikosi hicho.

Hata hivyo licha ya kufukuzwa kambini, Obua amegoma kuondoka akikiambia kituo kimoja cha redio: "Niko tayari kwa ajili ya mchezo huu mkubwa katika maisha yangu". Cranes lazima washinde mchezo dhidi ya Harambee Stars katika mchezo wa mwisho katika kundi J ili kujihakikishia nafasi ya kuingia katika michuano hiyo mwezi Januari mwakani.

Kukosekana kwa Obua wakati kikosi hicho kikijiandaa na mchezo mgumu kama huo, kunarejesha kumbukumbu za mwaka 1978 ambapo baba wa David, Denis, alipigwa marufuku kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kutokana na utovu wa nidhamu.

David ambaye anachezea klabu ya Hearts ya Scotland alikuwa hana uhakika wa kushiriki mchezo huo dhidi ya Kenya kutokana na jeraha la paja, sababu ambayo imetajwa na vyombo vya habari kuwa ilimfanya asisubiri mkutano wa rais.

Hatua yake ya kuondoka kambini imesababisha kuondolewa kambini mjini Kampala.

David Obua ni mmoja wa wachezaji muhimu wa Uganda, na wengi wana matumaini kuwa sakata hili litamalizika katika kipindi cha saa 24.