Clemente asema bado ni kocha

Kocha wa timu ya taifa ya soka ya Cameroon, Javier Clemente, amesema yeye rasmi ni mwalimu wa timu hiyo, hadi wakati mkataba wake utakapokwisha, au ikiwa shirikisho la soka nchini humo litaamua kuufupisha.

Mhispania Clemente, alishindwa kuiwezesha timu ya nchi hiyo, Indomitable Lions, kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2012.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Kocha Clemente akiwa na kocha msaidizi Omam Biyik

Hayo yamezua mjadala nchini Cameroon, kuhusiana na hatma yake, lakini yeye anasisitiza bado ni kocha wa timu ya taifa.

"Nitaendelea hadi nipate maelezo tofauti; nina mkataba, na ambao utaendelea hadi tarehe 30 mwezi Juni mwaka 2012," Clemente aliielezea BBC.

Chama cha soka cha Cameroon, Fecafoot, kililielezea shirika la habari la Reuters siku ya Alhamisi kwamba juhudi zimeanza za kumtafuta kocha ambaye ataendelea na kazi yake Clemente.

"Chama cha soka kimeongeza juhudi za kumtafuta kocha mpya kabla ya mwisho wa mwezi huu ili awe na nafasi ya kuiandaa timu kwa mechi za kufuzu kushirikishwa katika mechi za Kombe la Dunia mwaka 2014 na vile vile Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2013," Junior Binyam, msemaji wa Fecafoot alielezea.

Shirikisho linasisitiza kwamba kocha huyo alishindwa katika kazi yake ya kuiwezesha timu ya Indomitable Lions kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2012.

"Ni wazi kwa wote kwamba Clemente alishindwa kuwafikisha Lions katika Kombe la Mataifa ya Afrika mwezi Januari mwaka ujao, kufanyika katika nchi jirani za Gabon na Equatorial Guinea," Binyam alielezea.