West Brom yailaza Aston Villa 2-1

Bao la kwanza kabisa kwa Yohan Cabaye kuifungia Newcastle limeinyon'gonyesha Wigan baada ya kupoteza mechi yake ya sita ya mfululizo ya ligi.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Yohan Cabaye

Newcastle ilikuwa na wakati mgumu kutafuta nafasi huku Leon Best nusura aipatie timu yake bao la kuongoza kwa kichwa lakini mpira huo uliokolewa na mlinda mlango wa Wigan Ali Al Habsi.

Newcastle iliimarika lakini Wigan walionekana kwao walichokuwa wakitafuta ni sare hadi Cabaye alipofumua mkwaju wa yadi 20 na bao hilo likadumu hadi mwisho na kuipatia timu hiyo pointi 19 wakiwa nafasi ya nne sawa na Chelsea walio nafasi ya tatu.

Mabao mawili yaliyofungwa dakika za mwisho yameisaidia Sunderland kupata ushindi wake wa kwanza nje ya uwanja wao na kuiacha Bolton ikigaagaa bila pointi msimu huu katika uwanja wao wa nyumbani wa Reebok.

Stephane Sessegnon alikuwa wa kwanza kupachika bao baada ya kuachia mkwaju mkali uliompita mlinda mlango Jussi Jaaskelainen.

Darren Pratley alipata nafasi nzuri ya kusawazisha bao hilo lakini mlinda mlango Simon Mignolet alikaa imara na kuokoa.

Nicklas Bendtner aliihakikishia Sunderland ushindi na pointi tatu baada ya kupachika bao la pili kwa mkwaju wa yadi 10 baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Sessegnon.

Nayo Wolves ilibidi ifanye kazi ya ziada dakika za mwisho kuweza kusawazisha mabao mawili baada ya kuwa nyuma na kubanwa vilivyo na Swansea City na kumaliza mpambano huo kwa kufungana mabao 2-2 hali iliyompunguizia joto la moyo meneja wao Mick McCarthy.

Wenyeji hao hadi kipindi cha kwanza kilipomalizika walikuwa nyuma kwa mabao 2-0 na ilionekana dhahiri Wolves wakielekea kupoteza mchezo wa sita mfululizo wa Ligi Kuu ya England.

Danny Graham alikuwa wa kwanza kuwapatia wageni bao la kungoza na muda si mrefu Joe Allen akaipatia Swansea bao la pili.

Lakini mkwaju wa karibu wa Kevin Doyle ulifufua matumaini ya Wolvea kwa kuiandikia timu yake bao la kwanza na mkwaju wa Jamie O'Hara's uliinyima Swansea ushindi na kuisawazishia Wolves na hadi mwisho matokeo 2-2.

Na West Brom ikiwa nyuma kwa bao moja ilijipapatua na kuweza kushinda kwa mabao 2-1 dhidi ya Aston Villa. Aston Villa walilazimika kucheza wakiwa pungufu mchezaji mmoja baada ya Chris Herd kutolewa nje kwa kadi nyekundu katika hali iliyoonekana ni ya kutatanisha.

Darren Bent aliipatia bao la kwanza Aston Villa kwa mkwaju wa penalti kabla Herd kuoneshwa kadi nyekundu baada ya kumfanyia rafu Jonas Olsson ndani ya sanduku la hatari.

Chris Brunt alipoteza mkwaju wa penalti baada ya kufumua mshuti kubwa nje, lakini makosa hayo yalisahaulika haraka baada ya Olsson kusawazisha kwa kichwa kutokana na mpira wa kona.

Bao la pili lililowahakikishia ushindi West Brom lilifungwa na Paul Scharner baada ya kuunganisha mkwaju mkali wa kona.