Odinga: Kenya kuandaa Kombe la Dunia

Waziri Mkuu wa Kenya amesema nchi hiyo inaweza kuandaa mashindano ya kandanda ya Kombe la Dunia hivi karibuni.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Raila Odinga

Raila Odinga anataka nchi hiyo kuwa mwenyeji wa mashindano ya soka ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2019 kabla haijajaribu kuandaa mashindano ya Kombe la Dunia.

"Tutawekeza fedha zaidi siku zijazo katika kandanda nchi kwetu. Kusema kweli tunataka kujitokeza kuwania nafasi ya kuandaa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika," Odinga aliiambia BBC.

"Kenya ina uwezo na nafasi ya kuandaa si mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika lakini pia Kombe la Dunia."

Kenya ilikabiliwa na matatizo kadha ya kuandaa mashindano ya kimataifa kufuatia ajali ya mashabiki wa kandanda kukanyagana ambapo watu watano walikufa katika uwanja wa Nyayo mwaka jana.

Taarifa za awali zilisema mashabiki wanane walipoteza maisha yao lakini polisi wakatoa idadi nyingine ya watu waliokufa kuwa ni watano.

Bw Odinga amesema serikali ya Kenya itatengeneza miundo mbinu ya kandanda ili kutoa uhakikisho wa usalama kwa mashabiki hali itakayosaidia nchi hiyo kuweza kuandaa mashindano ya soka ya kimataifa.

Waziri Mkuu huyo alisema wanachukua hatua kuhakikisha viwanja vya soka nchini humo vipo katika hali ya usalama na vifaa vinaimarishwa.

"Iwapo mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika yanaweza kuandaliwa na nchi kama Burkina Faso, kwa nini Kenya isiweze? aliuliza Bw Odinga

Mkasa uliotokea mwaka jana ni ajali mbaya ya pili katika uwanja wa Nyayo katika kipindi cha miaka mitano.

Kijana mwenye umri wa miaka 15 alikufa wakati wa mechi ya kimataifa baina ya Kenya na Morocco mwezi wa Juni mwaka 2005.

Ahadi ya uchunguzi wa kifo hicho haikutolewa.