Tevez huenda akamshitaki Roberto Mancini

Carlos Tevez huenda akamshitaki meneja wa Manchester City Roberto Mancini kwa kumchafulia jina, kwa mujibu wa taarifa kutoka kambi ya mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentina.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Carlos Tevez

Siku ya Jumanne, Manchester City ilimtoza faini Tevez kwa kumkata mshahara wa wiki nne - kiasi cha paundi milioni 1 - kutokana na kile walichosema alikiuka maeneo matano tofauti ya mkataba wakati wa mchezo dhidi ya Bayern Munich mwezi wa Septemba.

Kukiukwa huko kwa mkataba kulikoelezwa na klabu ya Manchester City kunajumuisha, "kuwa tayari kucheza mechi yoyote ambayo mchezaji atateuliwa kushiriki kwa ajili ya klabu kama atakavyotakiwa na ofisa wa klabu".

Tevez ameshauriwa kwamba maoni aliyotoa Mancini baada ya mechi, ambapo alisema Tevez aligoma kucheza, kunamaanisha kumchafulia jina.

Msemaji wa klabu ya Manchester City amekiambia kipindi cha michezo cha BBC, hawasema chochote katika suala hilo lakini akaongeza mmiliki wa timu Sheikh Mansour na mwenyekiti Khaldoon Al Mubarak wanamuunga mkono Mancini kwa kauli moja.

Tevez, ambaye ana siku 14 za kukata rufaa kwa bodi ya klabu dhidi ya mashtaka yake, ameendelea kujitetea kwamba hakuna wakati wowote kwenye mchezo wa Ubingwa wa Ulaya nchini Ujerumani mwezi wa Septemba, aliambiwa ataingia kucheza na inaaminika anafikiria kuchukua hatua za kisheria.

Yeye pamoja na washauri wake wanaamini hakuna sababu hata moja iliyo sahihi kati ya hizo tano zilizotolewa na Manchester City na kwamba hazina uzito wa mashtaka ya kukiuka masharti ya mkataba, ambayo klabu ilichapisha katika mtandao wake siku ya Jumatano.

City imeamua kutorefusha adhabu ya kusimamishwa kwa wiki mbili kwa Tevez ambaye tayari ameshashatumikia.

Mchezaji huyo ambaye hajacheza tangu tarehe 21 mwezi wa Septemba wakati wa mechi ya Kombe la Carling dhidi ya Birmingham, kwa hiyo kimsingi anaweza kuchaguliwa kucheza mechi ya kuwania Kombe la Carling mzunguko wa nne dhidi ya Wolves siku ya Jumatano.

Lakini kuhama klabu hiyo mwezi wa Januari ni suala linaloonekana haliepukiki, huku Tevez akiwa anafanya mazoezi peke yake tangu aliporejea katika klabu hiyo baada ya kumaliza adhabu ya kufungiwa kucheza.