Rais Nkurunziza apata tuzo

Tuzo zilitolewa na shirika la Peace and Sport, ambalo nia yake ni kuwahamasisha watu kwamba michezo ni mbinu nzuri ya kujumuisha pamoja jamii, na kuleta hali ya amani duniani.

Tuzo hizo zilianzishwa mwaka 2008, na hutolewa kila mwaka katika mkutano wa dunia kuzungumzia juu ya amani na michezo.

Haki miliki ya picha L.Materra
Image caption Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza akihojiwa na Alex Mureithi

Rais Nkurunziza alisema; "Katika miaka ya hivi karibuni, michezo imekuwa muhimu katika kuwaunganisha pamoja raia wa Burundi".

"Tumefanya mikakati ya kuhakikisha michezo ni chambo kinachoweza kutumia katika kuimarisha umoja na uhusiano mzuri katika jamii na kupata amani nchini Burundi, na tunaamini kwamba kupitia michezo, vijana wanaweza kuchangia maendeleo ya kijamii, na hivyo kuimarisha uchumi na familia kote Burundi."

Huwezi kusikiliza tena

Shirika la East Africa Cup, nalo lilipata tuzo kwa kuwaleta pamoja vijana kati ya miaka 11 hadi miaka 16 katika shughuli za michezo, sio tu katika mataifa ya Afrika Mashariki, mbali pia kusini mwa Afrika.

Shughuli zake ni katika mataifa ya Zimbabwe, Zambia, Burundi, Rwanda, Uganda, Tanzania, Kenya na Sudan ya Kusini.

Mbali na soka, shirika liliweza kupanga pia mashindano ya voliboli, na voliboli ya walemavu wanaotumia viti vya magurudumu.

Shirika hili kufikia sasa limeanzisha mikakati mbalimbali ya kupata amani duniani hasa katika mataifa ambayo bado hayana utulivu, au yaliyowahi kujikuta katika hali hiyo, kama vile Ivory Coast, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Israel, Palestina, Timor, Colombia na Haiti.

Mwanzilishi na rais wa shirika, Joel Bouzou, anayeshikilia medali ya Olimpiki katika mchezo wa pentathlon, sasa hivi ni katibu mkuu wa chama cha mchezo huo duniani, na vile vile mshauri wa mwanamfalme wa Monaco, Albert wa pili.

Joel Bouzou pia alitangaza kwamba mataifa kumi yamethibitisha yatashiriki katika mashindano ya kwanza ya kimataifa ya shirika hilo, katika kutumia mashindano ya tennis ya mezani, kufanyika Qatar, kati ya tarehe 21-22 mwezi Novemba, kama juhudi za kupata amani.

Mataifa hayo ni Korea ya Kaskazini, Korea ya Kusini, Uchina, Japan, India, Pakistan, Urusi, Marekani, Ufaransa na wenyeji Qatar.