Wenger asifu uwezo wa Van Persie Arsenal

Meneja wa Arsenal Arsene Wenger amemsifu nahodha Robin van Persie ambaye amemwita "asiye wa kawaida" baada ya kufunga mabao matatu peke yake wakati Arsenal ilipoifumua Chelsea 5-3 katika uwanja wa Stamford Bridge.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Arsene Wenger

Wenger amesema: "Robin kwa sasa hashikiki na ubora wake unaamanisha yupo katika kikosi chenye uchu wa kushambulia na kutafuta nafasi. Akili anayotumia uwanjani na usahihi wake katika kumalizia hauna mfano."

Ameongeza: "Tulikuwa tukihitaji ushindi hapa na tumeendelea kushinda. Nadhani tuna kikosi kizuri na moyo wa hali ya juu kwa sababu wakati tulipokuwa tumelala mabao 2-1 muda mfupi kabla mapumziko hali ilikuwa ngumu.

"Lakini tulikianza kipindi cha pili kwa mtazamo tofauti wa kwenda mbele kushambulia na kwa upande wa ngome tulikuwa afadhali zaidi kipindi cha pili kuliko ilivyokuwa kipindi cha kwanza.

Nina matumaini timu inaweza kuimarika katika kujiamini kutokana na kiwango ilichoonesha na tutaweza kuendelea kuimarika kila siku."

Wenger amepongeza kuimarika kwa kikosi cha Arsenal kwa sababu wachezaji wapya waliojiunga muda mfupi kabla ya kufungwa dirisha la usajili mwezi wa Agosti wameweza kuzoea philosophia yake na mbinu za uchezaji.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Andre Villas-Boas

Naye kocha wa Chelsea Andre Villas-Boas amekanusha madai kwamba uchunguzi unaoendeshwa na Chama cha Soka cha England dhidi ya tuhuma zinazomkabili John Terry za maneno ya kibaguzi aliyomtolea mlinzi wa QPR Anton Ferdinand wakati Chelsea ilipofungwa na QPR katika mechi iliyopita ya ligi, umeathiri kiwango cha nahodha wake huyo.

Kocha huyo wa zamani wa klabu ya Porto amesisitiza kamwe hataacha kutumia mtindo wa timu yake wa ushambuliaji licha ya makosa ambayo safu ya ulinzi iliyafanya walipoadhibiwa na Arsenal.