Steven Gerrard aumia kifundo cha mguu

Liverpool inasubiri kufahamu ukubwa wa jeraha la Steven Gerrard baada ya nahodha huyo kuonekana na magongo ya kutembelea huku kifundo cha mguu kikiwa kimefungwa plasta.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Steven Gerrard aumia tena

Gerrard hakucheza siku ya Jumamosi, Liverpool ilipoilaza West Brom mabao 2-0 kutokana na kuumia kifundo cha mguu, ikiwa ni hivi karibuni tu alipona matatizo ya nyonga.

Alipigwa picha akitoka hospitali akiwa na magongo na kulikuwa na taarifa alitolewa maji katika kifundo hicho cha mguu.

Kuna wasiwasi Gerrard huenda asiweze kucheza katika mechi ambayo England itapambana na Hispania pamoja na Sweden mwezi wa Novemba.

Nahodha huyo alisafiri na kikosi cha Liverpool hadi Black Country siku ya Ijumaa, lakini baadae kifundo cha mguu wake kikaanza kuvimba siku ya Jumamosi asubuhi na hivyo kutangazwa hataweza kucheza dhidi ya West Brom.

Meneja wa Liverpool Kenny Dalglish amesema: "Steven alikuwa mawazoni acheze mechi hiyo. Ghafla kifundo cha mguu kikafura.

"Hatutampotosha yeyote. Tutafahamu vyema ukubwa wa tatizo lake siku ya Jumatatu au Jumanne.

"Jee atakuwa tayari kuichezea England? Siwezi kujua. Tatizo la sasa hivi halihusiani na kuumia kwake siku za nyuma - ni maambukizo tu.

"Nadhani ni sawa kuwa na usaha kinywani kwako."

England itacheza na Hispania katika uwanja wa Wembley siku ya Jumamosi Novemba 12 na itakabiliana na Sweden katika uwanja huo huo siku tatu baadae.

Lakini kuumia kwake hivi sasa itakuwa ni pigo kubwa kwa mashabiki wa Liverpool wakati timu hiyo inajiandaa kukabiliana na Swansea tarehe 5 Novemba.

Gerrard hakucheza mechi za kumalizia msimu uliopita na zile za kuanza msimu huu kutokana na matatizo sugu yaliyokuwa yakimsumbua ya nyonga.

Kiungo huyo alirejea uwanjani akiwa mchezaji wa akiba katika mechi dhidi ya Brighton tarehe 21 Septemba katika mechi ya Kombe la Carling.

Tangu wakati huo akamudu kucheza tangu mwanzo mechi mbili za Ligi Kuu ya England dhidi ya Manchester United na Norwich.

Dalglish pia alieleza mlinzi Jamie Carragher hakucheza dhidi ya West Brom kutokana na matatizo ya goti.