Arsenal yashindwa kuinyoa Marseille

Image caption Wachezaji wa Arsenal walinda ngome yao

Licha ya kucheza nyumbani, timu ya Arsenal wameshindwa kuifunga timu ya Olympic Marseille ya Ufaransa ilikujihakikishia tiketi katika hatua ya 16 bora ya ligi ya mabingwa.

Hatua ya Mkufunzi Arsene Wenger kumuacha njee ya kikosi chake nahodha Robin van Persie kulionekana kuwapunguzia miamba ya Arsenal motisha.

Washambulizi wa Arsenal hawakuonekana kwamba ni tishio katika ngome ya wageni wao Marseille katika mechi hiyo.

Badala yake ni Olympic Marseille ndio waliokuwa mwiba katika ngome ya Arsenal huku Jordan na Andre Ayew wakikosa nafasi kadhaa za kuiadhibu Arsenal nyumbani kwao Emirates.

Licha ya sare hiyo Arsenal bado inaongoza kundi F wakiwa na alama nane . Olympic Marseille ni ya pili na alama saba.

Barcelona 4 - 0 Viktoria Plzen

Kwengineko mabingwa watetezi Barcelona ya Uhispania waliwatwanga Viktoria Plzen ya Jamhuri ya Ucheki kwa magoli 4-0.

Mchezaji bora duniani Lionel Messi aliwaonyesha kivumbi wenyeji wao kwa kufunga mabao matatu. Cesc Farbregas aliipatia Barca bao la tatu katika dakika ya 72.

Hii ni mara ya 14 kwa Lionel Messi kufunga mabao matatu katika mechi moja tangu aanze kuichezee Barcelona .

Kwa ushindi huo Barcelona inakuwa timu ya kwanza kujikatia tiketi ya kuingia katika hatua ya 16 bora ambayo ni mechi za muondoano.