Chelsea yashutumu nyimbo za kebehi

Chelsea imelaani nyimbo za kebehi kutoka kwa mashabiki wake zilizokuwa zikimhusu mlinzi wa QPR Anton Ferdinand wakati timu hiyo ilipopambana na Genk katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya siku ya Jumanne na kutoka sare ya bao 1-1.

Haki miliki ya picha PA
Image caption John Terry

Mashabiki hao waliosafiri na timu ya Chelsea mara kwa mara walisikika wakiimba kuhusu Ferdinand, anayedai alitamkiwa maneno ya kibaguzi na nahodha wa Chelsea John Terry katika uwanja wa Loftus Road tarehe 23 mwezi wa Oktoba.

Msemaji wa Chelsea amesema katika taarifa aliyoitoa: "Nyimbo hizo za kebehi kamwe hazikubaliki na hatuzipuuzi."

Meneja wa Chelsea Andre Villas-Boas amesisitiza hakusikia nyimbo hizo.

"Nilikuwa nafuatilia mchezo ulivyokuwa ukiendelea," alisema.

Tukio hili limetokea katika siku ambayo Polisi wameanza rasmi uchunguzi wa tuhuma za Terry kutumia lugha ya ubaguzi dhidi ya Ferdinand wakati QPR ilipoilaza Chelsea bao 1-0.

Haijafahamika iwapo klabu ya Chelsea itakabiliwa na adhabu yoyote kutokana na nyimbo hizo.

Terry alikuwa mchezaji wa akiba ambaye hakucheza katika mechi dhidi ya Genk kwenye uwanja wa Cristal Arena wakati timu yake ilipopoteza nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Akizungumzia kiwango cha timu yake katika mechi hiyo, Villas-Boas amesema timu yake ilikosa ukakamavu langoni.