Upasuaji Redknapp wafanikiwa

Upasuaji wa kuzibua misipa inayotoririsha damu katika moyo wa meneja wa Tottenham Harry Redknapp umefanikiwa.

Image caption Harry Redknapp upasuaji wake wa moyo wafanikiwa

Redknapp mwenye umri wa miaka 64 alilazwa hospitali siku ya Jumanne usiku kwa ajili ya vipimo na upasuaji umefanyika Jumatano

Redknapp anatazamiwa kuruhusiwa kutoka hospitali ndani ya saa 48 lakini hakuweza kusafiri kuelekea Urusi na kikosi cha Tottenham kwa mechi ya Ligi ya Europa dhidi ya Rubin Kazan siku ya Alhamisi.

Mwenyekiti wa Spurs Daniel Levy amesema: "Tumefarijika upasuaji umekwenda vyema. Tunajua Harry atataka kurejea kazini haraka, lakini jambo la muhimu afanye hivyo pale tu atakapokuwa amepona kabisa."

Meneja wa West Ham Sam Allardyce alishawahi kufanyiwa upasuaji wa moyo mwaka 2009 na muda mfupi tu afya yake ikatengemaa na meneja wa zamani wa Liverpool Graeme Souness mwaka 1992 alifanyiwa upasuaji wa moyo lakini muda mfupi baade aliporudi kazini timu yake ikaondolewa katika michuano ya Kombe la FA.

Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson aliwekewa kifaa cha kupimia mapgo yake ya moyo mwaka 2004, lakini siku iliyofuata akarejea kazini.

Mameneja wengine wa vilabu vikubwa waliwahi kukumbwa na matatizo makubwa ya moyo, Joe Kinnear alifanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo hali iliyomlazimisha asiweze kuendelea kuifundishaha Newcastle mwaka 2009.

Meneja wa zamani wa Liverpool na baadae Aston Villa Gerard Houllier aliwahi kufanyiwa upasuaji wa dharura wa moyo mwaka 2001 uliyochukua muda wa saa 11 baada ya kupata matatizo ya moyo wakati wa mapumziko Liverpool ilipopambana na Leeds.

Alirejea kuifundisha Liverpool baada ya miezi mitano ya kujiuguza, lakini alifanyiwa upasuaji kama huo msimu uliopita baada ya kusumbuliwa tena na matatizo ya moyo alipokuwa katika klabu ya Villa na kwa sasa ameamua kupumzika kabisa.