Adebayor arejea timu ya taifa

Ade Haki miliki ya picha bbc
Image caption Adebayor amebadili uamuzi wa kustaafu

Emmanuel Adebayory amerejea kuichezea timu yake ya taifa baada ya kuhakikishiwa usalama wake na chama cha soka cha Togo (FTF).

Adebayory, 27, alikutana na maafisa wa FTF siku ya alhamisi kuzungumzia wasiwasi wake huo.

Mshambuliaji huyo anayechezea Tottenham amesema yupo tayari kuichezea timu yake ya taifa wiki ijayo dhidi ya Guinea Bissau katika mchezo wa kufuzu kucheza Kombe la Dunia mwaka 2014.

"Ninafurahi kusema kuwa narejea kuichezea Togo, na niko tayari kuanzia wiki ijayo dhidi ya Guinea Bissau." Adebayor ameiambia BBC.

Mchezaji huyo alistaafu kuichezea timu yake ya taifa baada ya shambulio dhidi ya timu hiyo ambapo watu wawili waliuawa wakati wakielekea katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2010.

Adebayor amesema maehakikishiwa na uongozi wa mchezo huo kuwa nchi itarekebisha hali ya usalama kwa wachezaji wote katika michezo ijayo.