Pienaar aitwa tena Bafana Bafana

Pienaar
Image caption Steven Pienaar alizongwa na majeraha

Kiungo wa Tottenham Steven Pienaar amejumuishwa katika kikosi cha Afrika Kusini kwa ajili ya mechi za kirafiki mwezi huu dhidi ya Ivory Coast na Zimbabwe.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 29, ambaye hivi karibuni amepona majeraha yake, amejumuishwa katika kikosi cha wachezaji 28.

Alikosa kipindi cha mwisho cha mechi za kufuzu kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika mwezi Septemba kutokana na jeraha la goti na nyonga.

Siyabonga Nontshinga, Musa Bilankulu, Granwald Scott na George Libese waliitwa kwa mara ya kwanza.

Nahodha wa Bafana Bafana, Pienaar, ni mmoja kati ya wachezaji tisa wanaochezanje ya nchi kuitwa katika kikosi cha kocha Pitso Mosimane.

Kiungo wa Crystal Palace Kagisho Dikgacoi pia ameitwa tena baada ya kupona.

Afrika Kusini itapambana na Ivory Coast katika mchezo wa kila mwaka wa kombe la Nelson Mandela, Novemba 12.

Bafana Bafana itasafiri kwenda Harare kupambana na majirani zao Zimbabwe siku tatu baada ya mchezo huo, katika kujiandaa kufuzu kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika 2013 na Kombe la Dunia 2014.