Newcastle yazitia hofu "timu kubwa"

Hekaheka katika lango la Everton
Image caption Hekaheka katika lango la Everton

Newcastle imendeleza rekodi yake ya kutopoteza mchezo tangu msimu msimu huu wa ligi ulipoanza wakati Ryan Taylor bao lake la pili lilipoizamisha kabisa Everton.

Jack Rodwell alifanikiwa kufunga bao kwa kichwa baada ya kuunganisha mkwaju wa kona na kuirejeshea matumaini Everton na kulikuwa na dalili za Everton wangeweza kupatiwa mkwaju wa penalti kipindi cha pili wakati Dan Gosling alipounawa mpira.

Lakini kikosi cha Alan Pardew kilisimama imara na kujihakikishia kubakia nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi.

Newcastle kwa sasa haijapoteza mchezo katika ligi tangu walipopoteza mchezo kwa kufungwa mabao 3-0 mwezi wa Mei dhidi ya Liverpool msimu uliopita, lakini wanakabiliwa na mtihani mgumu katika mechi zao tatu zijazo.

Robin van Persie akiwa amefunga bao la kwanza na kutengeneza mengine mawili, aliisaidia Arsenal kushinda mfululizo michezo minne iliyopita ya ligi kuu ya England. Arsenal iliizamisha West Bromwich Albion mabao 3-0.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Robin van Persie

Arsenal hawakuwa katika hali yao ya kawaida kabla ya kupata bao, lakini walibadilika baada ya kuwa mbele kwa mabao 2-0, bao la kwanza likifungwa na Van Persie na la pili likawekwa wavuni na mlinzi Thomas Vermaelen baada ya kupokea pasi ya Van Persie.

Arsenal iliendelea kumiliki kipindi cha pili na Vermaelen, Gervinho na Aaron Ramsey nusura wangefunga mabao.

Bao la tatu la Arsenal lilipachikwa na Mikel Arteta.

Manchester United imeendeleza furaha ya miaka 25 ya umeneja wa Sir Alex Ferguson katika klabu hiyo, baada ya kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Sunderland.

Haki miliki ya picha pa
Image caption Wes Brown alijifunga mwenyewe dhdi ya Man United

United walipata bao lao hilo kwa kuzawadiwa na mchezaji wao wa zamani Wes Brown aliyejifunga mwenyewe kwa kichwa alipokuwa katika jitihada za kuokoa mpira wa kona.

Manchester United walibadilika kipindi cha pili na kucheza vizuri lakini hawakuweza kuongeza bao jingine.

Javier Hernandez alipiga kichwa mpira uliokuwa ukielekea wavuni lakini ukaokolewa katika mstari wa lango na Wayne Rooney pamoja na Patrice Evra walijaribu mikwaju lakini iliokolewa.

Akiwa amefunga bao lake la sita la msimu huu wa ligi Frank Lampard alifanikiwa kuipatia ushindi finyu Chelsea wa bao moja kwa bila dhidi ya Blackburn inayokabiliwa na mzozo wa mashabiki kumkataa meneja.

Lampard alifunga bao hilo kwa kichwa baada ya kupokea pasi ya pembeni ya Branislav Ivanovic.

Image caption Mfungaji wa bao pekee la Chelsea Frank Lampard

Mashabiki wa Blackburn walikodi ndege iliyokuwa ikivinjari juu ya anga ya uwanja wa Ewood Park ikiwa na bango linalomchagiza meneja Steve Kean atimuliwe.

Na chagizo zikiendelea kupamba moto dhidi ya Kean, Yakubu na Grant Hanley walikosa nafasi nzuri za kufunga na pia mlinzi Gael Givet mkwaju wake ukagonga mwamba.

Mabao mawili aliyofunga Darren Bent na jingine la Gabriel Agbonlahor yameisaidia Aston Villa kuzoa pointi tatu dhidi ya Norwich.

Image caption Darren Bent akishangilia bao

Aston Villa wakicheza uwanja wao wa nyumbani ndio walikuwa nyuma kwa bao moja lililofungwa kutokana na mkwaju maridadi wa adhabu ya moja kwa moja uliopigwa na Anthony Pilkington, lakini bao hilo lilisawazshwa muda mfupi na Bent.

Agbonlahor baadae akatumia makosa ya Leon Barnett kurudisha pasi nyuma na kuipatia Villa bao la pili kabla ya kumtengenezea nafasi ya kupachika bao la tatu Bent.

Steve Morison aliipatia Norwich bao la pili kwa kichwa.

Nayo Liverpool ikicheza katika uwanja wao wa Anfield ilibanwa na Swansea City na kwenda sare ya kutofungana.

Mlinda mlango wa Swansea Micel Vorm alifanya kazi ya ziada kuwanyima wenyeji bao dakika za mwisho baada ya kuokoa mkwaju wa beki Glen Johnson aliouchia kutoka yadi 20, lakini Andy Caroll mwanzoni mwa mchezo alipoteza nafasi nzuri ya kufunga bao.