Muhammad Ali ahudhuria maziko ya Frazier

Muhammad Ali na mabondia maarufu walihudhuria ibada ya mazishi ya bingwa wa zamani wa uzito wa juu duniani Joe Frazier mjini Philadelphia siku ya Jumatatu.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Joe Frazier enzi za uhai wake katika masumbwi

Baadhi ya mabondia maarufu wa zamani waliohudhuria mazishi hayo ni pamoja na Larry Holmes, Mike Tyson na kiongozi wa wanaharakati wa kupigania haki za binadamu mchungaji Jesse Jackson walitoa heshima zao za mwisho katika kanisa la Enon Tabernacle Baptist.

Frazier alishinda medali ya dhahabu mwaka 1964 katika michezo ya Olimpiki na alikuwa bingwa wa masumbwi wa uzito wa juu duniani kuanzia mwaka 1968 hadi 1973.

Lakini Frazier umaarufu wake unazungumzwa zaidi kutokana na mapambano yake ya kukata na shoka dhidi ya Ali katika miaka ya 1970.

Na katika risala ya rambirambi iliyokuwa ya kusisimua, Mchungaji Jackson alitaka jiji la Philadephia kumtukuza na kumjengea heshima Frazier, akimlinganisha kwa umaarufu na mcheza sinema mashuhuri Sylvester Stallone, ambaye sanamu yake imewekwa katika jiji hilo.

Rocky ni mtu ambaye hakuwepo, alisema Jackson. "Rocky kamwe hakuonja damu yake. Rocky hakuwahi kukabiliana na Ken Norton. Kamwe hakupambana na Ali. Halikadhalika hakuwahi kuchapana na Larry Holmes.

"Joe anastahiki kuheshimika ,ni mtu wa kupigiwa mfano kwa sababu ya kupenda familia, Joe wa kawaida aliyekuwa na vitu vingi vya ajabu."

"Ataendelea kuwa jirani yetu. Ataendelea kubakia mwenzetu kanisani. Ataendelea kubakia mtu kutoka mitaani, kwa hiyo Philadelphia itakuwa imejiwekea sifa kwa kumheshimu Joe Frazier, lakini hili lisichelewe kufanyika."

Alipoulizwa na waandishi wa habari Frazier akumbukwe vipi, Mchungaji Jackson alijibu: "Kama bingwa mashuhuri wa ngumi na binadamu wa kutukuka. Bingwa wa ngumi kwa sababu aliwahi kushinda medali ya dhahabu, kwa sababu hakuirithi hiyo medali, aliifanyia kazi kubwa."

Wakati huo huo binti wa Frazier, Renar Frazier-Martin - mmoja kati ya watoto 11 na wajukuu 28 wa Frazier - alisema atamkumbuka baba yake kila mara alikuwa mstari wa mbele kwa watoto wake, hasa kwa sababu unapokuwa na watoto 11, ni kazi ngumu. Lakini kila mara alikuwa nasi nyumbani, wajukuu wake na familia nzima."

Katika ibada hiyo ya mazishi iliyochukua muda wa saa mbili, Tyson, mfanyabiashara Donald Trump na muigizaji Mickey Rourke walituma salamu za rambirambi kwa mkanda wa video.