Villas-Boas akanusha mashtaka ya FA

Meneja wa Chelsea Andre Villas-Boas amekanusha mashtaka dhidi yake yaliyowasilishwa na Chama cha Soka cha England- FA, kutokana na maneno aliyomtamkia mwamuzi Chris Foy baada ya timu yake kulazwa bao 1-0 na QPR.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Andre Villas-Boas akanusha mashtaka dhidi yake

Villas-Boas amekiri alikuwa "mkali sana" kwa mwamuzi Foy, aliyewatoa nje kwa kadi nyekundu wachezaji wawili wa Chelsea na kuwaonesha wengine saba kadi ya manjano.

Villas-Boas, alishatakiwa siku ya Ijumaa kwa utovu wa nidhamu baada ya klabu yake kupigwa faini na FA ya paundi 20,000.

Taarifa ya klabu ya Chelsea imesema: "Meneja anakanusha mashtaka dhidi yake na amewasilisha utetezi wake kwa FA."

Wakati wa mchezo huo, Jose Bosingwa alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumuangusha Shaun Wright-Phillips wakati akiwa anajiandaa kufunga bao, wakati Didier Drogba yeye alioneshwa kadi nyekundu kwa kucheza rafu ya kuingia kwa miguu miwili alipokuwa akiwania mpira dhidi ya Adel Taarabt.

Chelsea baadae ilitozwa faini baada ya kukiri mashtaka ya kushindwa kuwadhibiti wachezaji wake.

Akizungumza baada ya kupoteza mechi hiyo, Villas-Boas, ambaye huu ni msimu wake wa kwanza akiwa meneja wa Chelsea alisema: "Mwamuzi alishindwa kuchezesha vizuri, alikuwa ovyo sana. Na kwa sababu hiyo imetukosesha ushindi.

"Nilizungumza naye baada ya mchezo na nilikuwa mkali sana. Sijali kama yupo sawasawa au la.

"Kila mtu anaweza kuwa na siku mbaya, lakini hii si siku mbya kwetu. Ilikuwa siku nzuri kwetu na mbaya kwa mwamuzi."