Capello asifia damu changa England

Kocha wa timu ya taifa ya kandanda ya England Fabio Capello ana matumaini makubwa sasa amevumbua vipaji vipya kabla ya michuano ya Ubingwa wa Ulaya mwaka 2012 maarufu Euro 2012 baada ya ushindi wa bao 1-0 mfululilizo katika uwanja wa Wembley dhidi ya Hispania na Sweden.

Image caption Fabio Capello ana matumaini na damu changa England

Capello alimuanzisha Jack Rodwell wa Everton na beki wa Tottenham Kyle Walker katika mechi dhidi ya Sweden siku ya Jumanne na aliendelea kumtumia kiungo wa Manchester United Phil Jones kumiliki sehemu ya kati ya uwanja kama alivyofanya Jumamosi walipoilaza Hispania.

"Nilikuwa natafuta kitu kipya na nimekipata," alisema Capello.

"Nimekipata kitu kipya kwa Rodwell, Walker na Jones. Hii inafurahisha sana."

Kuhusu kiungo Rodwell, mwenye umri wa miaka 20, beki wa kulia Walker, aliye na umri wa miaka 21, na Jones, aliye na miaka 19, Capello ameongeza: "Kiufundi ni wazuri sana, wananguvu na wana kasi ya ajabu. Hili ni jambo muhimu kwa soka ya kisasa."

Capello, ambaye atajiuzulu katika nafasi yake ya ukocha baada ya patashika za kuwania ubingwa wa Ulaya mwakani zitakazoandaliwa kwa pamoja na Poland na Ukraine, amefurahi sana kwa matokeo wanayoendelea kuyapata na ana matumaini ya kumaliza mwaka wa 2011 bila kupoteza mchezo.

Na bao la kujifunga wenyewe kutoka kwa Daniel Majstorovic katika dakika ya 22, liliipa ushindi England dhidi ya Sweden.