Mkataba wa Hiddink wakatizwa Uturuki

Guus Hiddink amekatishiwa mkataba wa kuifundisha timu ya taifa ya Uturuki baada ya nchi hiyo kushindwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Euro mwaka 2012.

Haki miliki ya picha 1
Image caption Guus Hiddink akatishiwa mkataba na Uturuki

Shirikisho la Kandanda la Uturuki - TFF - limesema wamefikia makubaliano kumaliza mkataba wa mwalimu huyo wa zamani wa Chelsea, ambao ulikuwa umalizike mwakani.

Uturuki ilipoteza kwa jumla ya mabao 3-0 dhidi ya Croatia baada ya kwenda sare ya kutofungana mechi ya pili siku ya Jumanne.

Hiddink, mwenye umri wa miaka 65, alichukua kazi ya kuifundisha timu ya taifa ya Uturuki mwezi wa Agosti mwaka 2010 na nchi hiyo ilishika nafasi ya pili katika kundi A.

Hiddink alishawahi kuwa mwalimu wa timu za taifa za Uholanzi, Korea Kusini, Australia na Urusi, pamoja na vilabu vya PSV Eindhoven, Real Madrid na Chelsea.

Taarifa rasmi iliyotolewa na TFF katika mtandao imesema: "Tungependa kumshukuru Bw Guus Hiddink kwa kazi yake wakati akiifundisha timu yetu ya taifa, na tunamtakia kila la kheri katika kazi yake siku za usoni."

Katika mahojiano kabla ya mechi siku ya Jumanne alisema alitazamia kumaliza kufanya kazi na Uturuki na akaongeza: "Nilifanya kazi kwa ajili ya kuijenga timu kwa siku za mbele lakini nadhani hii itakuwa mechi yangu ya mwisho na timu hii - ukweli ndio huo."

Hiddink, anayeaminika ni mmoja wa mameneja hodari wa kandanda, inasemekana bado anahitajika sana na vilabu kama Paris Saint-Germain ya Ufaransa na Anzhi Makhachkala zimeonesha tamaa ya kutaka kumchukua.