Mwanariadha wa Kenya akatwa miguu

Mwanariadha
Image caption Wakenya ni wanariadha maarufu duniani

Mwanariadha wa mbio ndefu kutoka Kenya aliyepotea kwa siku mbili katika baridi kali nchini Marekani, amekatwa miguu yake.

Marko Cheseto, 28, ni mmoja wa wanariadha kadhaa kutoka Kenya walioshiriki katika mbio za nyika na uwanjani katika chuo kikuu cha Alaska Anchorage UAA. Taarifa za kukatwa miguu ya mwanariadha huyo ziliripotiwa na wavuti wa Chuo Kikuu cha UAA, Idara ya Riadha siku ya Jumatatu.

Chiseto alionekana kama saa moja usiku katika jengo la chuo kikuu UAA Novemba 6, ikiwa ni Jumapili usiku, wakati theluji ikianza kuanguka katika mji huo. Watu wanaoishi naye walitoa taarifa za kupotea kwa mwanariadha huyo kesho yake asubuhi. Kupotea kwa mwanariadha huyo kulisababisha msako mkali wa kumtafuta katika jiji hilo.

Kuganda

Cheseto alipatikana mapema siku ya Jumatano nje ya hoteli moja iliyopo karibu na chuo kikuu. Alikuwa amevaa viatu vya michezo, koti jepesi na suruali ya jeans, lakini hakuwa na kofia au hata gloves za mikononi. Alikuwa amepatwa na baridi kali na miguu yake na mikono kuganda.

Meneja wa hoteli aliliambia gazeti la huko kuwa wakati Cheseto alipopatikana, waganga hawakuweza kumvua viatu vyake kwa sababu vilikuwa vimeganda kwenye miguu ya mwanariadha huyo.

Maafisa wa UAA wamesema mikono ya Cheseto inatazamiwa kupata nafuu, lakini maeneo yake ya miguu ilipigwa na baridi kali mno na kulazimika kukatwa. Anatazamiwa kusalia hospitali kwa muda kwa ajili ya matibabu zaidi, wamesema maafisa wa UAA.

Mafanikio

Polisi wa chuo kikuu walimhoji Cheseto mara baada ya kupatikana na kusema alipatwa na "janga binafsi" alipopotea. Mamlaka zilifahamu kuwa alikaa muda wote huo akiwa nje kwenye baridi.

Cheseto, mbali na kupata mafanikio yake kwenye riadha, amepewa tuzo ya mafanikio yake kielimu wakati akiwa kwenye chuo hicho, ambapo anasoma uuguzi na uwezo wake umekuwa wa hali ya juu, kwa mujibu wa chuo hicho.

Hata hivyo muda wake chuoni umezongwa na mikasa. Rafiki wake wa karibu William Ritekwiang wanayetoka eneo moja nchini Kenya la Kapenguria, alijiua mwezi Februari.

Wawili hao walikuwa miongoni mwa wakimbiaji kadhaa waliosaidia chuo kikuu hicho katika mbio za nyika na za uwanjani.