Wenger huenda akang'atuka mwezi wa Mei

Arsene Wenger amebainisha huenda msimu huu ukawa wa mwisho kwake katika klabu ya Arsenal.

Haki miliki ya picha a
Image caption Arsene Wenger atumbua jipu huenda akaondoka Arsenal

Wenger, mwenye umri wa miaka 62, ambaye amebakisha miaka miwili kabla ya mkataba wake kumalizika, aliliambia gazeti la L'Equipe ataangalia upya nafasi yake mwishoni mwa msimu.

"Kitu ambacho ni kigumu ni kule kuhisi kuna kitu kinamalizika. Kwangu mimi, kwa sasa tunazungumzia masuala ya muda mfupi, huo ndio ukweli," alisema.

"Lakini iwapo itakuwa mimi au mtu mwengine, haitabadilisha kitu. Mtu atakayechukua nafasi yangu anahitaji kujengewa msingi utakaomwezesha kuifanya kazi kwa mafanikio zaidi," aliongeza meneja huyo wa Arsenal.

Wenger amekuwa meneja wa Arsenal tangu mwaka 1996, akiiongoza timu hiyo kunyakua mataji matatu ya Ligi Kuu ya England na mataji manne ya Kombe la FA, lakini hata hivyo hajawahi kushinda kombe tangu mwaka 2005.

Mwezi wa Septemba, mmiliki wa Arsenal Stan Kroenke alisisitiza mustakabali wa Wenger upo mikononi mwake mwenyewe, na ataamua lini anataka kuondoka.

Alipoulizwa iwapo ataendelea kuifundisha klabu hiyo msimu ujao, Wenger kocha wa zamani wa Monaco alijibu: "Tutaangalia mambo yatakavyokuwa msimu huu ukimalizika."

Meneja huyo wa Arsenal pia amekiri kuwapoteza wachezaji Cesc Fabregas aliyekwenda Barcelona na Samir Nasri aliyejiunga na Manchester City ilikuwa ni hatua ngumu kwake.

"Kwa mara ya kwanza nilipoteza wachezaji vijana, ambao walikuwa wanakomaa. Nilihangaika. Inauma kupoteza wachezaji muhimu ambao uliwekeza sana," alisema.

Wenger mwezi wa Agosti mwaka 2010 alisaini mkataba wake wa sasa unaomalizika mwaka 2014. Na ni hivi karibuni mwezi wa Septemba, alizungumzia kuendelea kubakia Arsenal kwa "miaka mingine 14 ijayo."